HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 06, 2023

GST NDIYO MOYO WA SEKTA YA MADINI- WAZIRI MAVUNDE

•Aahidi kuipa  kipaumbele GST

•GST yatajwa kuwa ni moja ya kinara wa Maabara Bora ya Utafiti Madini Barani Afrika


Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Taasisi ya Jiolojia na Ufafiti wa Madini Tanzania (GST) ndiyo Moyo wa Sekta ya Madini na ni Taasisi inayotegemewa na Wizara ya Madini na Sekta ambata kama Sekta ya Maji, Kilimo na Ujenzi.

Mavunde ameyasema hayo baada ya kukutana na kuzungumza na watumishi wa GST Septemba 4, 2023, jijini Dodoma ikiwa ni kikao chake cha kwanza baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko.

Amesema, kwa kuwa GST inafanya tafiti mbalimbali na kupelekea kugundua migodi ya wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo, ameahidi kuipa kipaumbele taasisi hiyo baada ya kuonekana inamchango mkubwa kwenye sekta hiyo.

"Kulingana na historia GST ni kinara wa utoaji wa taarifa za masuala ya Jiolojia Barani  Afrika hivyo hakikisheni mnaweka mikakati ya kufanya taasisi hii iwe bora zaidi katika sekta ya madini," amesema Mavunde.

"Dunia kwa sasa inahitaji Madini ya Kimkakati ikiwemo Kinywe, Lithium na Nikeli kwa ajili ya mahitaji ya Teknolojia ya kisasa na ifikapo mwaka 2050 inategemewa kuwa mahitaji ya madini hayo yatakuwa mara miatatu zaidi ya yalivyo kwasasa," amesema Mavunde.

Aidha, Mavunde ameitaka GST kutengeneza mashirikiano na taasisi zingine za utafiti wa Madini duniani kwa lengo la kupata uzoefu, ujuzi na uwezo wa taasisi wa kupata vifaa vya kisasa zaidi na kuwa na Maabara bora Barani Afrika na kuifanya taasisi hiyo kuwa sehemu ya  utambulisho wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya GST Prof. Justinian Ikingula amesema jukumu kubwa la GST ni kufanya utafiti wa jiosayansi kwa lengo la kubaini rasilimali zilizopo ardhini ikiwa ni pamoja na aina za miamba sambamba na madini yanayopatikana kwenye miamba hiyo katika maeneo mbalimbali ya nchini.

Prof. Ikungula ameongeza kuwa, Taarifa za jiosayansi zinazokusanywa na GST ndizo kichocheo kikubwa cha uwekezaji na ukuaji wa Sekta ya Madini nchini ambapo utekelezaji wa majukumu hayo yameifanya GST kuwa kitovu cha taarifa za msingi za jiosayansi ambazo kwa nyakati tofauti zilipelekea gunduzi za migodi mbalimbali ya madini hapa nchini.

Naye, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amewasilisha mada ya mwenendo mzima wa shughuli za Utafiti ambapo amesema lengo la tafiti zinazofanywa na GST ni kuibua maeneo mapya yenye madini na hatimaye kuanzishwa kwa migodi mipya ya uchimbaji wa madini.

Tafiti za jiosayansi ambazo zimefanywa na GST ndizo chanzo cha kuanzishwa kwa migodi mbalimbali nchini kwa kutumia taarifa zake ikiwemo Geita Gold Mine (GGM), Bulyanhulu Gold Mine, Twiga Gold Mine, Nyanzaga Gold Mine, Shanta Gold Mine - Singida, Migodi ya Makaa ya Mawe na sehemu nyingine zenye uchimbaji mdogo na wa kati.



No comments:

Post a Comment

Pages