Na John Marwa
Klabu ya Simba imekuja na programu kabambe ya kuibua vipaji na mashabiki wapya kuanzia ngazi ya shule za msingi na kuendelea, hii ikiwa ni mara baada ya kuhitimisha zoezi la ukusanyaji vipaji kwa vijana chini ya miaka 15, 17, 18 na 20 Wasichana kwa Wavulana.
Huu ni mchakato wa kuendelea kujijenga ikiwa ni miongoni mwa Klabu kubwa Barani Afrika, wakiamini kwa kufanya hivyo basi watakuwa wanathibitisha ukubwa wao na kuendeleza mchezo wa soka kwa manufaa ya Taifa kupitia programu hiyo.
Hatua hiyo ni baada ya uongozi wa klabu hiyo kuja na Programu maalumu kutoka kwenye jopo la Makocha wa timu za vijana kutembelea shule zote Tanzania kwa kuipa jina la (Back to School).
Akizungumza na waandishi wa habari, leo jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Simba SC , Iman Kajula, amesema wameamua kurudi mashuleni kwa makocha wa timu za vijana kutembelea katika shule siku za michezo ili kuwaweka karibu watoto na Klabu yao.
Amesema wanatambua katika shule kuna vipaji na wanaenda huko kuibua wachezaji wapya lakini pia kuwaandaa mashabiki wa Simba wa baadae kupitia programu hiyo.
“Programu hiyo itakuwa endelevu kutembelea shule zote hapa nchini , huku makocha wetu wa vijana kufanya programu zao, lakini pia siku za mechi watoto katika shule mbalimbali watapewa nafasi ya kuja uwanjani kusapoti timu yao.
Amesema Simba kwa kushirikiana na wabia wao (taasisi za mabank) kuhakikisha wanakuwa na Akaunti za watoto ili wanapofungua wanakuwa sehemu ya mashabiki.
“Wabia wetu wamekubali hilo na sasa mzazi anapokwenda kumfungulia Akaunti anakuwa sehemu ya uanachama wa Simba, tumeenda mashuleni kwa sababu elimu na michezo inawafanya watoto wetu kuwa na utimamu wa mwili (Afya ya akili) na kujenga ushirikiano wenyewe kwa wenyewe na nidhamu,” amesema Kajula.
Naye Meneja wa programu za vijana wa Simba, Patrick Rweyemamu amesema baada ya kufanikiwa kupata timu ya vijana kuanzia U-17, 18, 19 na 20 sasa wanaenda katika shule za msingi na kindagate kwa ajili ya kuibua vipaji vya watoto.
Amesema miaka ya sasa watoto wamepoteza hamu ya kucheza mpira wa miguu kwa sababu ya changamoto za viwanja kuwa duni, sasa Simba wameamua kurudisha mapenzi ya kupenda kucheza na kuibua vipaji.
“Hii haitakuwa faida kwa Simba pekee bali ni kwa Taifa letu, tunapotengeneza programu hii inasaidia kuibua vipaji kuanzia chini na baadae itakuwa rahisi kupata wachezaji wazuri na kuleta manufaa kwa timu zetu za taifa za kike na kiume,” amesema Rweyemamu.
No comments:
Post a Comment