Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Ephraim Mafuru, akifafanua jambo wakati wa mkutano na
Wahariri na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam ambao ni muendelezo wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kutoa taarifa za utendaji kazi na mikakati yao.
Na John Marwa
Mashirika ya Serikali zaidi ya 17 yametajwa kuongoza kwenye orodha ya wadaiwa sugu wa Vituo vya Mikutano vya Kimataifa vya Arusha (AICC) na Julius Nyerere (JNICC), ambavyo vinazidai Taasisi za Serikali zaidi ya Sh. Bilioni 7.4.
Orodha hiyo imebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa AICC, Ephraim Mafuru, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 14, 2023 jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kutoa taarifa za utendaji kazi na mikakati ya maendeleo.
Amesema wana shida kubwa ya watu kulipa madeni, kwani hadi sasa wanazidaia taasisi na wateja zaidi ya Billion 7.4 huku taasisi za Serikali zikiongoza katika orodha hiyo ya wadaiwa sugu.
"Tuna shida kubwa ya watu kulipa madeni, mpaka tunaandaa ripoti hii, AICC na JICC ilikuwa inadai taasisi zote na wateja Sh. Billion 7.4. Bahati mbaya kati ya wadau wenye madeni makubwa ni Taasisi za Serikali.
"Ni ngumu kwa Mkurugenzi Mkuu kwenda kumdai Katibu Mkuu, ingawa kwenye mashirika binafsi tunawazuia ikiwa hawajalipa hawaingii hapa, lakini kuna njia ambazo tunatumia tumeishirikisha bodi yetu na Katibu Mkuu na hapa Waziri ameshatoa taarifa hizi taasisi zinazodaiwa zilipe madeni.
"Tunamshukuru Waziri Mkuu akiwa anafunga Bunge la Bajeti katika hotuba yake alitoa maelekezo, na mimi naomba ninukuu hapa na niwaombe hasa wakuu wa taasisi kama mimi tulipe madeni ili taasisi zetu ziweze kukua kimapato ziweze kujiendesha kwa faida," amesema Mafuru.
"Taasisi nyingine zinatangaza faida kubwa sana, yaani kuna mtu anatangaza kupata Sh. bilioni 300 alizotengeneza, kumbe hata madeni halipi. Hii hapana, tutafika mahali tutamuomba TR, atusaidie, kwamba kabla mtu hajatangaza faida yake, awe amelipa kwanza madeni. Naomba Sekretarieti huu ujumbe umfikie TR, kwamba AICC tutafika mahali tutapiga stop, kama ahujalipa hauingii kwenye kumbi zetu," alisisitiza.
Aidha, aliongeza ya kwamba AICC inaamini kuwa, Tanzania ina kila kitu tunachoweza kushindana katika uchumi wa mikutano, kwani nchi jirani wana miundombinu ya majengo peke yake, lakini hawana kitu kingine cha kuweza kuishinda Tanzania.
"Kwa kuzingatia upekee wa Tanzania kuna baadhi ya mikutano ambayo ilikuwa haijawahi kuja Afrika, lakini ikaja kwa mara ya kwanza na inakuja Tanzania, mwaka ujao tuna mkutano unaitwa Esperanto, ni lugha ya kimataifa haijawahi kuja Afrika lakini itakuja Tanzania Agosti 2024.
"Kutakuwa na wageni zaidi ya 3,000, lakini pia jana tumepewa taarifa na kikao cha Waziri wa Maliasili, Angela Kairuki, kuna timu ilikwenda Chile, ambako Tanzania imeshinda kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Vyama vya Wafuga Nyuki Duniani watakaokuja Tanzania mwaka 2027 ambapo taarifa zinasema watakuwa watu zaidi ya 7,000.
Mafuru alibainisha kwamba, AICC imejipanga kwa sababu wana maeneo ya kutosha ya kujenga Kituo cha NTICC, ili hiyo mikutano iweze kuja Tanzania.
Aidha ameishukuru Serikali kwa kuridhia mradi huo, kwa sasa wapo kwenye kuandika mpango na kujiridhisha kifedha ili waweze kuanza utekelezaji.
No comments:
Post a Comment