HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 16, 2023

Omuka Hub, NDI yatoa mafunzo kwa wanawake

 Na Mwandishi Wetu, Bukoba


SHIRIKA la Omuka Hub ambalo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Marekani National Democratic Institute - (NDI) wameandaa majadiliano kwa Jukwaa la Wanawake katika Siasa, kujadili mapendekezo ya Kikosi Kazi na Maazimio ya Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama Vya Siasa uliofanyika Septemba 11 hadi 13, 2023 mkoani Dar es Salaam.


Majadiliano hayo yameandaliwa chini ya uratibu wa Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira huko wilayani Bukoba mkoani Kagera ambapo amesema lengo ni kumuunga mkono maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha uwakilishi wa wanawake kwenye siasa.


"Mjadala juu ya ushiriki wa wanawake katika siasa katika ngazi zote kuanzia kitongoji hadi Taifa umefanyika Bukoba, Mjini na umehudhuriwa na washiriki 100 kutoka makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo viongozi wa dini, siasa, wakina mama viongozi , wakuu wa mashirika/NGOs na wengine.


Lugangira amesema maazimio ya mjadala huo yanakwenda kuwa chachu katika utekelezaji wa maono ya Rais Samia ya kuimarisha uwakilishi wa wanawake katika siasa. 


Aidha, amesema maazimio hayo yatawasilishwa kwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kupitia  Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina hiyo. 


"Washiriki wa semina hii wamempongeza Rais Samia kwa hotuba nzuri aliyotoa wakati anafungua Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama Vya Siasa kwani imeeleza uhalisia na inatoa dira jinsi ambavyo shughuli za siasa zinapaswa kufanyika nchini ili kudumisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa," amesema. 


Mbunge huyo ambaye amejipambanua katika kuinua wananchi wa kada mbalimbali amesema washiriki wamempongeza Rais Samia katika kuongoza nchi, hasa kwa kuanza kutekeleza map anayoiongoza kwa kutekeleza sehemu kubwa ya mapendekezo ya Kikosi Kazi.


Lugangira amesema washiriki wa semina hiyo wameridhishwa na maazimio ya washiriki wa mkutano maalum ulioandaliwa na Baraza la Vyama vya Siasa na Ofisi ya Msajili.


Kwa upande wake Msajili Msaidizi, Nyahoza amempongeza Mbunge Lugangira kwa ubunifu wake mkubwa wa kuandaa majadiliano hayo ambayo yamehusishaa Jukwaa la Wanawake katika Siasa kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Maazimio ya Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama Vya Siasa katika ngazi ya jamii. 


Nyahoza amewapongeza washiriki kwa mjadala mzuri na amechukua maoni yao ambayo yatafanyiwa kazi. "Kikubwa zaidi nimefurahia kukutana na washiriki kutoka ngazi ya jamii ambao wameonesha uelewa mkubwa na masuala ya ushiriki wa wanawake katika siasa," amesema. 


Msajili Msaidizi Nyahoza ametumia nafasi hiyo kuliomba Shirika la NDI kuendelea kushirikiana na Mwanziishi wa Shirika la Umuka Hub ili mafunzo hayo yafike kila kona ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Pages