HABARI MSETO (HEADER)


October 22, 2023

JMAT, Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Palestina waziomba Jumuiya za Kimataifa kuingilia kati Vita ya Israel na Palestina

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kushirikiana na Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Palestina wameziomba na kuzitaka Umoja wa Mataifa (UN) na Jumuiya za Kimataifa zihakikishe usitishwaji wa vita kati ya Israel na Plestina.
Akizungumza na wanahabari jijini humo Mwenyekiti wa JMAT Taifa Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum amesema kadhia ya vita ya Israel na Palestina imekuwa ni kadhia ya muda mrefu Mashariki ya Kati kwamba Dunia imeshuhudia mara kadhaa umwagikaji wa damu kwa pande zote mbili.

"Hata hivyo kwa upande wa Palestina tumeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi yao. Yanayotokea hivi sasa katika ardhi ya Palestina ni uvunjifu wa haki za Binadamu na Uvunjifu wa sheria za kimataifa, kama kupiga mabomu nyumba za Ibada, kupiga mabomu hospitali na vituo vya afya, kupiga makazi ya raia na hatimaye kuua raia wasio na hatia hasa wanawake na watoto na kupiga na kuharibu huduma za msingi za kibinadamu kama maji na umeme," amesema Sheikh Dkt. Alhad Mussa na kuongeza,

" Jambo hili limetuhuzunisha sana kama wapenda Amani duniani, pia ifahamike kwa jamii kwamba hivi si vita vya kidini moja kwa moja na visitugawe kati ya Waislam na Wakristo na watu wa dini nyingine mbalimbali. Aidha wanaouawa ni pale ni Waislam, Wakristo, pengine na wasiokuwa na dini,".

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa JMAT Taifa Askofu Dkt. Israel Ole-Gabriel Maasa amesema mambo hayo ni mambo ambayo hayakubaliki kwa watu wastaarabu.

Kwamba dini za Ukristo na Uislam pamoja na dini nyingine zote kwa ujumla hazikubaliani na uharibufu wa namna hiyo.

"Hivyo basi, tunaziomba na kuzitaka mamlaka husika hasa Umoja wa Mataifa na Jumuiya za Kimataifa zihakikishe usitishwaji wa vita hivyo mara moja pamoja na kuhakikisha huduma za kibinadamu hasa maji, umeme, dawa na huduma nyingine zinarejeshwa mara moja," ameeleza Askofu Dkt. Maasa.

Kadhalika ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuangalia kiini cha tatizo hilo na hivyo kupata ufumbuzi wa kudumu na amewaomba pia wadau na wapenda amani wote duniani kuzidi kupaza sauti zao dhidi ya uhalifu huu wa Kivita Mashariki ya Kati.

No comments:

Post a Comment

Pages