HABARI MSETO (HEADER)


October 12, 2023

Rais Samia ataka kasi utekelezaji makubaliano India

Na Selemani Msuya


RAIS Samia Suluhu Hassan, amewaagiza wasaidizi wake wote kusimamia utekelezaji wa makubaliano ambayo serikali imeingia na nchi ya India katika ziara ya kitaifa aliyoifanya kuanzia Oktoba 8 hadi 11 nchini humo.

Rais Samia ametoa maagizo hayo ndani ya ndege baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.


Alisema safari hiyo imekuwa na mafanikio makubwa, ila tafsiri sahihi itaonekana iwapo kila mtu atatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa maslahi ya taifa.


"Nashukuru Mungu tumeenda tumerudi salama, tumejadiliana kuhusu miradi mingi, tunapaswa kwenda kusimamia utekelezaji, ili faida ya safari ionekane, naomba hili likafanyika,"alisema.


Akiwa nchini India Rais Samia alisema mikakati ya serikali yake ni kuhakikisha ifikapo 2025 wawekezaji kutoka nje wawe wananchangia dola za Marekani bilioni 15 kwa mwaka kutoka dola za Marekani bilioni 5 za sasa.


Aidha, kiongozi huyo aliwahakikishia wawekezaji na wafanyabishara wa nchi hiyo kuwa Tanzania ni nchini nzuri ya kuwekeza na kwamba hawatajutia.


Katika ziara hiyo ambayo Rais Samia aliambatana na mawaziri saba wa Tanzania Bara na Zanzibar na wafanyabiashara, hati za makubaliano 15 zisainiwa huku 10 ikihusisha serikali na mitano sekta binafsi. 


Pia kupitia ziara hiyo Rais Samia alitunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nerhu (JNU) cha nchinj India akiwa ni mwanamke wa kwanza na kiongozi wa tatu kutunukiwa shahada hiyo.


Viongozi wengine ambao wametunukiwa shahada hiyo na JNU ni Rais wa Urusi Vladimir Putin na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe.


No comments:

Post a Comment

Pages