HABARI MSETO (HEADER)


October 13, 2023

Shirika la Amend lapongezwa kukamilisha mradi wa Usalama Barabarani


Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Rehema Kasimu (wa pili kushoto), akimpatia cheti cha kutambua mchango wa Mwalimu wa Shule ya Msingi Usagara Faraja Mwajike kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya usalama barabarani. Kushoto ni Meneja wa Amend Tanzania Simon Kalolo akishuhudia tukio hilo

 

Na Mwandishi Wetu, Tanga

 

HALMASHAURI ya Jiji la Tanga limetoa shukrani kwa Shirika la Amend baada ya kukamilisha Mradi wa Usalama Barabarani kupitia Mradi wa Tanga Yetu ambao umewezesha wananchi wa Jiji hilo kupata elimu kuhusu usalama barabarani sambamba na uboreshaji wa miundombinu katia shule za msingi.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mradi huo ambao ulianza mwaka 2019 na kumalizika mwaka 2023, Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahman Shillow amesema kwa kipindi cha miaka minne wamekuwa na Amend katika kushirikiana kuhusiana na suala zima la usalama barabarani.

 “Amend ni miongoni mwa mashirika yanayofanya kazi kwa ukaribu katika program ya Tanga Yetu , ni  miongoni mwa miradi 17 tuliyokuwa nayo katika miradi ya Tanga Yetu  na moja ya mradi huo ni mradi wa usalama barabarani.Katika mradi huu waliokuwa wamepata kazi ya kuusimamia na kuendesha ni Amend.

“Mradi huu umefika mwisho na umefanyika kwa miaka minne ukiwa unafadhiliwa na Shirika la Botna chini ya mradi wa Tanga Yetu na leo tumekuja kuwapa taarifa wadau tuliokuwa tunashirikiana nao tangu mwanzo kama.

“Ni mradi ambao umekuwa na mafanikio makubwa ndani ya miaka hii minne kwa kuhakikisha elimu ya usalama barabarani imetengamaa na imejitosheleza katika jiji letu la Tanga, kwasababu mradi huu pia uligusa uboreshaji wa miundombinu,”amesema Shiloo.

Amefafanua kuwa wameboresha miundombinu katika Shule ya Msingi Usagara, Chuda,   Mwazange na Mabawa katika maeneo mahususisi ambayo watoto wanaweza kupita kwa usalama na kuepuka kupata ajali za barabarani.

 “Elimu hiyo imetolewa ya kutosha katika Jiji la Tanga na zimetolewa kwa nyakati tofauti lakini hawakuishia hapo wametoa elimu kwa madereva zaidi ya 900 ambao nao walipewa elimu sahihi ya matumizi ya barabara lakini jinsi gani ya kumlinda mtumia barabara ili na yeye awe salama.”

Ameongeza kikubwa zaidi ambacho Amend walikifanya na kuvutia zaidi ni kuanzisha Mahakama Kifani ya Watoto iliyokuwa ikiendesha kesi za madereva waliovunja sheria za usalama barabarani na madereva hao  walihukumiwa.

Meya Shillow amesema Mahakama ya Watoto imewasaidia watoto hao kuwa na  ujasiri na kufahamu haki zao kuwa sheria za barabarani zipo na zinatakiwa zifuatwe na zinaweza kutolewa hukumu na watu wakahukumiwa.Pia amesema kupitia mradi huo kumekuwepo na mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uelewa wananchi.

 “Tunawashukuru Amend walitutengenezea mpango kazi wa Jiji letu la Tanga kuhusu suala zima la usalama barabarani, ni suala kubwa kwetu .Niwaambie tu Amend wamekuwa na sisi kwasababu tu ya kufadhiliwa na Foundation Botna na sasa mradi umekwisha.

“Jambo la kufurahisha mradi huu umekwisha lakini  Amend wamepata mfadhili mpya ambaye ni Serikali ya Uswiss ambao wameona umuhimu wa kuendelea na Amend katika Jiji la Tanga pamoja na Jiji la Dodoma ambako nako watapata huduma kama ambazo zimetolewa kwetu.

“Amend wanafanya kazi kwa uhalisia na linafanya kazi na watu wenye uhitaji, watu ambao wanahitaji kusemewe na sisi kama viongozi wa umma tunawasemea watoto wetu ili tujenge taifa nzuri lisilokuwa na watoto wenye ulemavu kwa miaka ijayo na ili tujenga taifa lenye upendo ni lazima tuwajali hawa watoto ikiwa pamoja na kuangalia usalama wao,”amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo amesema, mradi umefanikiwa kubadilisha mtazamo wa viongozi wa juu wa Jiji la Tanga kuhusu usalama barabarani.

Amesema kabla ya mradi huo kulikuwa na kiwango cha kawaida cha hatua, uratibu na dhamira ya kukabiliana na usalama barabarani huku akifafanua kila mdau alikuwa akifanya kazi yake tofauti tofauti.

“Kwa muktadha wa mradi huu, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa wadau na wakala mbalimbali kukutanishwa kuchangia maoni yao kuhusu usalama barabarani. Utengenezaji wa Mpango Kazi wa Usalama Barabarani kwa Jiji la Tanga uliofanywa na Amend …

“Uliozinduliwa na mkuu wa wilaya, na kuhushirikisha taasisi zote za serikali husika (wilaya, halmashauri ya jiji, barabara na polisi wa trafiki) walihusika. Mpango huo ni wa kwanza kabisa wa aina yake kwa Tanga.Umeweka dira ya usalama barabarani ya 2023-2030 na kuainisha mikakati ya kufanikisha hili.

“Pia unatumika kama ramani ya barabara kwa wadau wa usalama barabarani Tanga katika maendeleo ya sera (halmashauri ya jiji) na utekelezaji (wahandisi na trafiki).”

 Akieleza zaidi kuhusu mradi huo amesema tangu ulipoanza mwaka wa 2019 mpaka mwaka 2023 pamoja na mambo mengine kumefanyika uboreshaji wa miundombinu katika shule za msingi 11, ikiwa ni pamoja na njia za miguu, madaraja ya waenda kwa miguu, alama za barabarani, matuta, alama za pundamilia, na zaidi;

Amesema Amend kwa kushirikiana na Kikosi cha usalama barabarani wameendesha mafunzo kwa waendesha pikipiki zaidi ya 900 huku pia wakitekeleza Mahakama ya Watoto katika shule tano za msingi (Usagara, Mwanzange & Martin Shamba, Mwenge, Mwakizaro),

Aidha wametoa elimu ya usalama barabarani kwa zaidi ya watoto 12,000 wa shule za msingi, uwezeshaji wa mafunzo kwa Polisi wa Trafiki, kampeni ya uhamasishaji wa usalama barabarani ikijumuisha kampeni ya vyombo vya habari, ujumbe kupitia kwa maofisa wa maendeleo ya jamii na ujumbe kupitia wanasiasa wakiwemo madiwani,

Ameongeza pia wametoa mafunzo kwa maofisa wa Serikali 139, taasisi za elimu 14, wanafunzi 12,894, walimu 128, askari polisi 29 na madereva 1,220 wameguswa moja kwa moja na kutengeneza Mpango Kazi wa Usafiri Salama na Endelevu wa Jiji la Tanga.

No comments:

Post a Comment

Pages