Na Selemani Msuya
WAKULIMA wa Afrika wameshauriwa kutumia mbegu asili katika kilimo kwa kuwa nichangia salama kwa afya, uhuru wa chakula, kukuza uchumi na uhakika wa soko.
Ushauri huo umetolewa leo na Mratibu wa Mtandao wa Bioanuai Afrika (ABN), Dk Fassil Gebeyehu wakati akizindua Mradi wa Kuimarisha Mtandao wa Mifumo ya Mbegu (FMSS) inayosimamiwa na wakulima kwa uhuru wa chakula kwa upande wa Tanzania.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam katika makoa makuu ya Shirika la Envirocare, ambapo mratibu huyo amesema dunia inatakiwa kusisitiza kilimo cha kutumia mbegu asili kwani ndio salama kwa maisha ya watu.
Dk Gebeyehu amesema mradi huo unatekelezwa katika nchini tatu ambazo ni Kenya, Uganda na Tanzania na utamalizika Oktoba 2024, ambapo lengo kuu ni kuhakikisha mbegu asili zinapewa kipaumbele kwenye kilimo.
"Leo tumezindua Mradi wa Kuimarisha Mtandao wa Mifumo ya Mbegu inayosimamiwa na wakulima kwa uhuru wa chakula kwa upande wa Tanzania utatekelezwa na Mtandao wa Bionuai Tanzania (TABIO) na Shirika la Envirocare, tunaamini ndani ya mwaka tutapata mwelekeo kuhusu eneo hili, muhimu kwa maisha yetu, kwani mimi naamini usalama wa mbegu ni usalama wa maisha yetu," amesema.
Amesema ABN imekuwa ikitumia mbinu ya kukutana na jamii na kuielezea faida za matumizi ya mbegu asili, hivyo ni imani yake kuwa mradi huo utajikita katika kutoa elimu kwa makundi yote ili yaelewe umuhimu wake.
"Lengo kuu la jitihada hii ni kuimarisha mifumo ya mbegu inayosimamiwa na wakulima, kukuza uhuru wa chakula Kenya, Uganda, na Tanzania kwa kuwawezesha wakulima wa ndani, mradi unalenga kuongeza tofauti (anuai) ya mbegu, kuimarisha ushiriki wa jamii, na kuchangia kwenye uhakika na usalama wa chakula Afrika ya Mashariki, tukijikita kwenye elimu tutaweza kupata suluhisho,"ameongeza.
Amesema tafiti zilizofanyika zimeonesha wazi kuwa mbegu asili zinachangia uzalishaji mwingi, usalama wa chakula na soko la uhakika, hivyo ni vema nguvu ikaelekezwa huko.
Kwa upande wake Mratibu Mawasiliano, Ushauri wa ABN, Venter Mwongera amesema mradi huo unafadhiliwa na Bread for the World (Brot) na unatarajia kufukia makundi mbalimbali 2,000 ya wakulima, watunga sera 50 na wadau wa sekta hiyo 5,000 katika nchi husika.
Amesema ABN inatamani kuona mkulima mdogo ananufaika na kilimo na hilo litawezekana iwapo mbegu zao zitapewa kipaumbele kwenye Serikali na wadau wengine.
"Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), 2, 13 na 15 yanazungumzia uhakika wa chakula na mazingira, hivyo ili watu wasiwe na njaa ni vema tuungane pamoja kusisitiza kilimo cha mbegu asili kwani kina uhakika zaidi," amesema.
Venter amesema ili kampeni hiyo iweze kupenya kwa urahisi ni muhimu vyombo vya habari vinatumika, kwani ni nyenzo muhimu katika kufikisha ujumbe kwa jamii na wafanya maamuzi.
Aidha, mratibu huyo ameshauri wadau wa mbegu asili kuweka mkazo kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii ambapo kuna wafuatiliaji, hali ambayo itaongeza msukumo wa kampeni hiyo muhimu kwa maisha ya wanadamu.
Mratibu wa TABIO, Abdallah Mkindi amesema mradi huo umezinduliwa nchini, hivyo wataweka mkazo mkubwa wa kuhakikisha wanafikia makundi yote ambayo yanaweza kufanikisha mchakato mzima wa kuzifanya mbegu asili ziweze kutambulika na kuthaminiwa.
Mkindi amesema mbegu asili zimethibitika kuwa ni salama kwa afya ya binadamu, hivyo ujio wa ABN na miradi huo unafungua ukurasa mpya wa mapambano ambayo yatawezesha wakulima nchini kunufaika na mbegu hizo.
"Sisi TABIO na Envirocare tutashirikiana na wadau wote ambao kwa njia moja au nyingine wanashiriki kuhamasisha matumizi ya mbegu asili, ili serikali iweze kuweka mazingira mazuri yatakayofanywa mbegu hizi zitambulike kisheria na kisera," amesema.
Amesema mbegu za mkulima zinapitia changamoto kubwa ya teknolojia ambayo ndio imechukua nafasi, hivyo ni vema kila mpenda usalama wa chakula kuungana nao.
Naye Ofisa Program wa ABN, kutoka Envirocare Euphrasia Shayo amesema watakutana wadau kutoka serikali yaani watunga sera, mashirika yanayojihusisha na kilimo na wakulima ili dhamira ya kukuza sekta hiyo kupitia mbegu asili iweze kufikiwa.
"Sisi na TABIO tutahakikisha mbegu asili zinapewa msukumo kwa kutoa elimu kwa makundi yote," amesema.
Ofisa Uraghibishi na Uchechemuzi wa Kituo cha Bioanuai Afrika, Sabrina Masinjila amesema uwepo wa sera na sheria kuhusu mbegu za wakulima ambazo bado hazijapewa kipaumbele.
Pia Masinjila amesema uwepo wa sheria na sera utafanikiwa kwa haraka kwa elimu kutolewa zaidi hasa kwa makundi ya wakulima ambao wengi wapo vijijini.
Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, William Ernest amesema chuo hicho kimejikita kwenye utafiti wa mbegu asili kwa kuwa wanaona ni eneo muhimu kwa hatima ya mkulima na walaji.
Ernest amesema kukosekana kwa uhuru wa mbegu matokeo yake ni kukosekana kwa uhuru wa chakula, hivyo wameamua kutafiti eneo hilo ili uhuru wa chakula uwepo.
"Mbegu asili ni endelevu, salama na zinatoa uhuru wa chakula, lazima tupambane kwa pamoja kufanikisha kampeni hii," amesema.
Nao wakulima wa mbegu asili Yusuph Ndama kutoka kijiji cha Italagwe wilayani Gairo mkoani Morogoro na Deodatus Bajuta kutoka Karatu mkoani Arusha wamesema mbegu hizo ndio uhakika wa afya bora na endelevu.
Wakulima hao wamesema mazao yanayozalishwa kwa mbegu asili ni tiba ya magonjwa mengi na kuomba Serikali iweke mkazo kwenye eneo hilo.
No comments:
Post a Comment