HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 23, 2023

TBA kuwachukulia hatua za kisheria Wadaiwa Sugu, yawadai Wapangaji Sh Bilioni 7.8

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) umesema kuwa hadi sasa jumla ya fedha kiasi cha Sh bilioni 7.8 zinadaiwa kwa wapangaji wake zikiwemo taasisi za umma zinazotumia nyumba na majengo yake.

Akizungumza na wanahabari jijini humo Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro amesema kuwa wapangaji wote zikiwemo taasisi za umma zinatakiwa kuhakikisha zinalipa madeni yao kwa wakati kabla hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao.

 

"Kwa sasa TBA imeazimia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wapangaji wote tunaowadai, moja ya hatua zitakazochukuliwa ni kuwaondoa wadaiwa sugu kwa nguvu kwa kutumia dalali wa Mahakama ambaye amepewa zabuni hiyo kufanya kazi kwa niaba ya TBA. Mpaka sasa tayari dalali wa mahakama ambaye ni Twins Auction Mart amekabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa hatua zinazofuata na zoezi hili litafanyika kuanzia Desemba 1, 2023 katika Mikoa yote nchini." ameeleza Kondoro.

 

Aidha amesema, hatua hiyo itakwenda sambamba na kuwafungulia mashtaka wadai wote watakaondolewa katika nyumba na majengo hayo ili kuhakikisha kuwa fedha yote inayodaiwa inakusanywa.

 

Vile vile ameeleza juu ya maboresho yaliyofanyika kwenye mfumo wa kielekroniki. “Kuanzia tarehe 1 Desemba, 2023, tutaanza kutumia mfumo mpya wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Miliki za Serikali (GRMS) toleo la 2.Mfumo huu mpya utakuwa unatoza riba ya 20% kwa mpangaji atakae kaa zaidi ya miezi 3 bila kulipa kodi ya pango. Riba hiyo itaendelea kutozwa kila mwezi kwa kiwango mfuto (automatically) cha 20% mpaka deni lote litakapokamilika kulipwa” amesema Arch. Kondoro.

 

"Hadi kufikia Oktoba 31 mwaka huu TBA inadai zaidi ya Bilioni 7.8 za kodi ya pango kutoka kwa wapangaji wa nyumba na majengo yanayomilikiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) nchi nzima ambapo zaidi ya Bilioni 3.5 ni madeni ya Taasisi mbalimbali za Serikali." Amesema.

 

Kuhusiana na hatua ya kuwaondoa wadaiwa sugu kwa kutumia dalali wa Mahakama ambaye amepewa zabuni hiyo kwa niaba ya TBA; Arch Kondoro amesema kampuni ya udalali wa Mahakama ya Twins Auction Mart imeshakabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa kuanzia Desemba Mosi mwaka huu na hatua itakayofuata mara baada kuondolewa katika nyumba hizo kuwafungulia kesi za madai mahakamani wadaiwa hao ili kuhakikisha wanalipa madeni hayo.


"Madeni haya ni ya mwaka wa Fedha uliopita...Na Mikoa kinara ni taasisi za Umma katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya ambayo deni limefikia shilingi Bilioni 1.4......Nitoe rai kwa wapangaji wote zikiwemo taasisi za Umma kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati mara baada ya kupokea namba za kumbukumbu za malipo yaani control number ambazo hutumwa kwa kila mpangaji Kila mwezi kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS.)" Amefafanua.
 

Aidha, Arch. Kondoro ameeleza kuwa; Kuanzia Desemba 1, 2023, Wakala hiyo itaanza kutumia mfumo mpya wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Miliki za Serikali (GRMS) toleo la 2.
 

"Mfumo huu mpya utakuwa unatoza riba ya 20% kwa mpangaji atakae kaa zaidi ya miezi 3 bila kulipa kodi ya pango. Riba hiyo itaendelea kutozwa kila mwezi kwa kiwango mfuato (automatically) cha 20% mpaka deni lote litakapokamilika kulipwa. Utekelezaji huu ni kwa mujibu wa kifungu Na. 5.2 cha mkataba wetu wa upangishaji." Amesema.
 

Takribani nyumba 1716 zinazomilikiwa na TBA zimepangishwa kwa watumishi na viongozi wa Umma nchi nzima huku utekelezaji wa miradi hiyo ukiendelea nchi nzima na katika jitihada za kuepukana na ulimbikizwaji wa madeni ya pango TBA imekuja na ubunifu kwa miradi inayotekelezwa sasa kutumia vitasa janja (smartlock) kwenye majengo mapya ili kudhibiti malimbikizo ya kodi ya pango huku mpango huo wa kufunga vitasa janja ukidhamiriwa kutekelezwa katika nyumba za zamani.

No comments:

Post a Comment

Pages