NAIBU
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin
Rwezimula amefunga Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Ubora wa Elimu
ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) na kuwakutanisha
Wadau wa Elimu kutoka Nchi 10 za Afrika.
Akizungumza
wakati wa kufunga Kongamano hilo Jijini Dar es Salaam Dkt. Rwezimula
amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, wadau na
Taasisi mbalimbali zinazojihusisha na maswala ya Elimu katika kuboresha
mazingira ya Elimu nchini ili iweze kumkomboa Mtoto wa Kitanzania.
Dkt.
Rwezimula amesema kuwa Serikali hajajikita tu katika kutoa ahadi
mbalimbali juu ya Elimu bali imeendelea kuboresha mazingira ya Elimu kwa
kujenga madarasa na nyumba za walimu, kupitia mitaala, kiboresha sera,
Kuboresha uwezo wa walimu kwa kuwapa mafunzo ya mara kwa mara ili
kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kuwafundisha wa watoto kulinganana na
kasi ya mabadiliko ya Dunia inavyokwenda.
"Serikali
itaendelea kuhakikisha elimu nchini inakuwa bora na inayoweza kumkomboa
mtoto wa Kitanzania, na ili kufanikisha hilo tutashirikiana na wadau
mbalimbali kama TENMET na tunawapongeza kwa kongamano hili ambalo
linatoa chachu ya kufanya madiliko mbalimbali katika sekta ya elimu,"
amesema Dkt. Rwezimula.
Ameeleza
kuwa katika majadiliano yao wameweza kubainisha kuwa kunahitajika
kuongeza kasi ya utoaji wa mafunzo mbalimbali ya mara kwa mara kwa
walimu ili kuhakikisha elimu wanayowapa wanafunzi inakidhi matakwa ya
elimu bora ikiwa ni pamoja na kuwa na mitaala yenye kukidhi matakwa ya
Dunia ya sasa na kutoa mawanda mapana ya mtoto kujifunza kidigital na
kupewa nafasi ya kuonesha ujuzi na kipawa chake nje ya elimu ya
darasani.
Kwa
upande wake Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania TENMET Ochola Wayoga
amesema katika siku tatu za kongamano hilo wameweza kujadili kwa kina
maswala ya Elimu ikiwemo kujadili kuhusu maeneo ya kujifunzia,nyenzo za
kufundishia,kujifunza kwa njia za digital, changamoto za mimba za
utotoni,mitaala na sera ya elimu.
Nae Mwenyekiti
wa Bodi ya TENMET Faraja Nyalandu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano inaoutoa
kwa kwao pia amewashukuru wadau wote wa elimu na Taasisi mbalimbali za
ndani na nje ya nchi zilizotoa muda wao kushiriki katika kongamano hilo
la Kimataifa la Ubora wa Elimu.
Faraja
ameongeza kuwa Tenmet kipaumbele chake kikubwa ni kuhakikisha Tanzania
na Afrika kwa ujumla inakuwa na Elimu bora kulingana na Kasi ya
mapinduzi ya nne ya viwanda Dunia.
No comments:
Post a Comment