Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) John Mathew Mnali akizungumza kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari kuhusu Mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyofanya nchini Morocco na Saudi Arabia. Mkutano huo umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2023.
Na Selemani Msuya.
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesema ziara anazofanya Rais Samia Suluhu Hassan katika nchi mbalimbali duniani zimeongeza wawekezaji kwa kiwango kikubwa.
Kauli hiyo ya neema ya ziara za Rais Samia inatolewa na TIC, huku kukiwa na baadhi ya watanzania wanalalamikia ziara hizo kwa kile wanachodai kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ikulu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Uhamasishaji Uwekezaji, John Mnali amesema miaka miwili ya Rais Samia madaraka imefungua sekta ya uwekezaji jambo ambalo linatoa picha nzuri kuelekea 2025 ambapo wanatarajia wawekezaji wachangie shilingi trilioni 30 kwa mwaka.
Alisema uwekezaji katika ulimwengu wa sasa umetawaliwa na ushindani wa nchi zinazoendelea kuwekeza katika nchi zilizoendelea, hivyo ili nchi za dunia ya tatu kufanya vizuri ni lazima kujitangaza kama anavyofanya Rais Samia.
"Inawezekana ikatafsirika inavyotafsirika ila ili uweze kuvutia wawekezaji ni lazima utangaze fursa ulizo nazo kwa nchi zilizoendelea, kwani tafiti zinaonesha kuwa nchi hizo zinawekeza kwa nchi zilizoendelea pia, kusema kweli Rais Samia anatupaisha na kutufungulia njia sisi TIC tukienda kuwatafuta wawekezaji kazi inakuwa rahisi," alisema.
Mnali alisema kutokana na Rais Samia kuzunguka dunia kutangaza fursa zilizopo Tanzania katika kipindi cha Juni hadi Septemba 2023 TIC imesajili miradi 137 mpya ambayo itawezesha kupatikana ajira 86,900.
Mkurugenzi huyo alisema katika kipindi kama hicho mwaka 2022 walisajili miradi 86 ambayo iliwezesha kupatikana ajira 12,000, ila kwa ziara za hivi karibuni ongezeko limekuwa kubwa. Alisema uwekezaji ni sekta ambayo ina ushindani mkubwa, hivyo hakuna njia mbadala ya kufikia huko bila kuchangamana na watu, kama anavyofanya Rais Samia.
Mkurugenzi huyo alisema pamoja na ziara za Rais Samia kutangaza fursa zilizopo nchini, pia marekebisho ya sheria ya uwekezaji yamechangia ongezeko la wawekezaji hasa wazawa.
Alisema kwa sasa asilimia 49 ya wawekezaji nchini ni wazawa, hali ambayo imechangia na sheria nzuri iliyopo, hasa kwenye kipengele cha mtaji.
Pia tumeweka vivutio vingi na wawekezaji wameonesha kuridhishwa na imani yetu lengo la Rais Samia kuona mchango wa sekta hiyo kwa mwaka unafikia shilingi trilioni 30, ifikapo 2025 linaenda kutimia,"alisema.
No comments:
Post a Comment