Na Selemani Msuya, Dodoma
WAANDISHI wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini wamepatiwa mafunzo kuhusu Mikataba ya Kimataifa ya Uwekezaji ambayo imekuwa ikitekelezwa kwenye sekta tofauti.
Mafunzo hayo yametolewa jijini Dodoma na Mtandao wa Muungano wa Asasi za Kiraia zinazofanya Uchambuzi wa Sera za Uwekezaji na Biashara Tanzania (TATIC).
Akizungumza na waandishi hao Mkurugenzi Mtendaji wa TATIC, Olivia Costa Balilo wakati akifungua mafunzo hayo ya siku mbili, ambapo ameweka bayana kuwa kuna ombwe katika uandishi wa habari za mikataba ya uwekezaji baina ya nchi na nchi, hivyo kupitia mafunzo hayo anaamini kutakuwa na mabadiliko chanya.
Alisema Tanzania ni moja ya nchi ambayo imeingia mikataba ya uwekezaji na nchi nyingine, hivyo TATIC imeamua kutoa mafunzo ili kuwezesha jamii kupata taarifa za uhakika kuhusu eneo hilo.
"Tumeamua kutoa mafunzo haya kwa waandishi wa habari tukiamini ni kundi muhimu katika kutoa taarifa za uwekezaji wa kimataifa mfano Mikataba ya uwekezaji kati ya nchi mbili MIUMBI ambayo sisi Tanzania tumeingia au tunatarajia kuingia na nchi nyingine, iwapo nyie mtakuwa na uelewa ni wazi jamii kwa ujumla itapata elimu ya kutosha,"alisema.
Balilo alisema washiriki wa mafunzo watajifunza kuhusu mikataba ya uwekezaji wa kimataifa na uchumi wa kisiasa, mikataba ya uwekezaji na makubaliano, masuala ya sheria na uchumi na mengine.
Mkurugenzi huyo alisema pia mafunzo hayo wametoa kwa watendaji wa serikali hasa wizara zinahusiana na mikataba hiyo kama mambo ya nje, viwanda na biashara, sheria na katiba na taasisi zingine mtambuka.
Alisema iwapo wadau hao na waandishi watakuwa na taarifa kuhusu mikataba ya uwekezaji ni wazi kuwa kila pande itanufaika na kuondokana na dhana ya pande moja kunyonywa.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya TATIC, Wakili Steven Msechu alisema hadi sasa Tanzania imesaini mikataba 18 BITs(MIUMBI) na nchi mbalimbali ambayo inatekelezwa kwa hatua tofauti.
Wakili Msechu alisema MIUMBI kama ilivyo mikataba mingine ina faida na hasara zake, hivyo ametoa raia kwa nchi kuangalia wapi wanaweza kurekebisha ili nchi zote ziweze kunufaika.
"Sisi Tanzania tumeingia BIT na baadhi ya nchi kama Canada, Finland, Italia, Mauritius, China, Denmark, Switzerland, Uingereza, Sweeden, Ujerumani na Uturuki. Lakini pia zipo nchi kama Kuwait, Oman, Jordan, Afrika Kusaini, Zimbabwe, Korea na Misri," alisema.
Naye mtoa mada Dk Clement Mashamba alisema changamoto anayoiona katika BIT ni wahusika kushindwa kutafuta taarifa kwa kina, hali ambayo inapelekea madhara kwa nchi.
Dk Mashamba alisema iwapo kila anayepata nafasi kushiriki kwenye michakato ataweka uzalendo mbele na wazi kuwa manufaa yatapatikana.
No comments:
Post a Comment