HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 13, 2023

Hati Fungani ya NMB Jamii Yaandika Historia Kwa Kukusanya Tsh Bilioni 400

Historia imeandikwa katika Masoko ya Mitaji Afrika Mashariki, baada ya Hati Fungani ya NMB Jamii kukusanya Tsh Bilioni 400, ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya lengo lililokusudiwa.
 
Hati Fungani hiyo imekusanya jumla ya Tsh Bilioni 212.9 kwa fungu la Shilingi za Kitanzania na Dola za Kimarekani Milioni 73 kwa fungu la Dola za Kimarekani.
 
Matokeo haya yametangazwa rasmi wakati wa hafla ya kuiorodhesha Hati Fungani ya NMB Jamii katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mapema leo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA, Nicodemus Mkama alisema:

 

“Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ina jukumu la kuweka mazingira ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayowezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za kugharamia shughuli za maendeleo. Kadiri Taifa letu linavyosonga mbele katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 yaani the Third National Five-Year Development Plan (FYDP III) wenye dhima ya kujenga “Uchumi Shindani kwa Maendeleo ya Watu”, mahitaji ya rasilimali fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, hususani miradi endelevu na yenye matokeo chanya kwa jamii yanaongezeka.

“Ili kufanikisha azma hii, kunahitajika uwepo wa bidhaa za kutosha, bunifu ambazo zinaleta anuwai katika masoko ya fedha, ikiwa ni pamoja na hatifungani za kampuni kama Hatifungani hii iliyotolewa na Benki ya NMB”.

 

Aidha, uwepo wa bidhaa nyingi katika masoko ya mitaji unachangia utekelezaji wa Sera za Fedha (Monetary policy) katika Uchumi na Sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi (economic empowerment policy); kuongezeka kwa akiba hapa nchini; kupanuka kwa uwekezaji unaoleta ongezeko la ajira; mapato kwa njia ya kodi kwa Serikali; na kuinua kipato cha watanzania kwa ujumla.

Mkama aliendelea kueleza kuwa:

“Mnamo tarehe 31 Agosti 2023, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) iliidhinisha maombi ya benki ya NMB kuuza toleo la kwanza la hatifungani iitwayo Jamii Bond yenye thamani ya shilingi bilioni 75, ikiwa ni sehemu ya Programu ya Hatifungani ya Miaka Kumi yaani Medium Term Note Programme yenye jumla ya thamani ya shilingi trilioni moja (Tsh 1,000,000,000,000) itakayotolewa katika fedha mbalimbali.

 

“Hatifungani hii imeweka historia ya kuwa hatifungani kubwa zaidi yenye mlengo maalum (thematic bond) kutolewa nchini Tanzania na katika Ukanda Kusini mwa Jangwa la Sahara na ambayo imewezesha kupata fedha za kutekeleza miradi endelevu na yenye matokeo chanya kwa jamii.


Vilevile CPA, Mkama aliendelea kueleza kuwa, Idhini ilitolewa na CMSA baada ya benki ya NMB kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya utoaji wa Hatifungani kwa umma yaani Capital Markets and Securities (Guidelines for the issuance of Corporate Bonds); uwepo wa Muundo wa Hatifungani yaani Jamii Bond Framework ulioandaliwa na benki ya NMB kwa kushirikiana na Taasisi ya Uendelezaji wa Sekta za Fedha Barani Afrika (FSD Africa) na kukidhi matakwa ya Kanuni za Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji yaani International Capital Markets Association – (ICMA) na kupata ithibati kutoka kwa kampuni ya Sustainalytics ya nchini Uingereza, yenye utaalam kuhusu miradi endelevu kwa maendeleo ya jamii.

 kwa namna ya pekee napenda kutambua mchango wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (European Union) hapa nchini, kwa kujengea uwezo wa kitaalamu wafanyakazi wa Mamlaka na hivyo kuwezesha kuwa na ujuzi na weledi katika masuala ya hatifungani zinazokidhi matakwa  endelevu na matokeo chanya kwa jamii”.

 

Mauzo ya Hatifungani ya NMB (NMB Jamii Bond) yalifunguliwa tarehe 25 Septemba 2023 na kufungwa tarehe 27 Oktoba 2023, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 212.94 kimepatikana, ikilinganishwa na shilingi bilioni 75 zilizotarajiwa kupatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 284. Kufuatia kiasi kilichopatikana kufikia shilingi bilioni 212.94, CMSA imeidhinisha Benki ya NMB kutumia kiasi chote kilichopatikana kutokana na uwepo wa mahitaji ya kutosha, kugharamia miradi endelevu na yenye matokeo chanya kwa jamii.

 

Mauzo ya hatifungani hii yamekuwa na mwitikio chanya unaoashiria kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu uwekezaji katika masoko ya fedha hapa nchini, ambapo asilimia 98.7 ya wawekezaji walioshiriki ni wawekezaji mmoja mmoja na asilimia 1.3 ya wawekezaji ni kampuni na taasisi”.

 

Aidha, asilimia 99.9 ya wawekezaji ni wawekezaji wa ndani na asilimia 0.1 ni wawekezaji wa nje. Kwa upande wa kiasi kilichopatikana, asilimia 53.8 inatoka kwa wawekezaji mmoja mmoja na asilimia 46.2 inatoka kwa kampuni na taasisi. Aidha, asilimia 57.4 ya kiasi kilichopatikana inatoka kwa wawekezaji wa ndani na asilimia 42.6 inatoka kwa wawekezaji wa nje ya nchi.

 

Ushiriki wa wawekezaji mmoja mmoja wa ndani ni hatua muhimu katika kuongeza ukwasi katika soko (liquidity); na utekelezaji wa Mpango wa Huduma Jumuishi za Kifedha yaani National Financial Inclusion Framework wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha. Hivyo, tuna kila sababu ya kuipongeza benki ya NMB na wadau wote walioshiriki katika kuwezesha mafanikio haya. Hongereni Sana!!.

 

Kwa upande wake akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya Hati Fungani hiyo na kuiorodhesha DSE, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, amesema: “NMB Jamii Bond ilikuwa imegawanyika katika mafungu mawili, fungu la kwanza likihusisha Shilingi za Kitanzania na fungu la pili la Dola za Kimarekani, ambako kote tumevuka lengo la makusanyo, kwa upande wa Shilingi tukipata Bilioni 212.9  kutoka Bil. 100 za lengo na upande wa Dola tukikusanya Milioni 73 badala ya Milioni 15.
 
“Kwa mantiki hiyo, thamani ya jumla ya fedha zilizopatikana kutokana na NMB Jamii Bond ni Sh. Bilioni 400, ambazo ni mara tatu zaidi ya lengo tulilokuwa nalo” amebainisha Bi. Zaipuna huku akiwahakikishia wateja zaidi ya 5,600 walionunua Hati Fungani hizo kuwa pesa zao ziko mikono salama.
 
“Tunawashukuru wateja wetu na wawekezaji wote kwa kutuamini na kusimama pamoja nasi katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii,” amesema Bi. Zaipuna.
 
Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa hafla hiyo aliipongeza NMB kwa kuweka rekodi ya Bilioni 400 za mauzo ya Hati Fungani hiyo.
“Hati Fungani ni fursa muhimu kwa jamii kunufaika kwa njia mbili za kuweka akiba, lakini pia kufanya uwekezaji wenye faida kubwa. Bond ni mkopo ambao taasisi ya fedha inakopa kwa wananchi. NMB ingeweza kwenda kukopa BoT au benki za nje, lakini ikachagua kukopa kwa wananchi kupitia mdhamana wao ambaye ni CMSA na inarejesha kwa riba kubwa ya asilimia 9.5.
 
“Rekodi hii ya mauzo inaweza kuwa ya kushangaza kwa taasisi zingine, lakini kwa NMB hili sio la kushangaza kutokana na ufanisi wake, ikitajwa mara 10 na Majarida ya Euromoney, Global Magazine, African Bankers na mengine kuwa ni Benki Bora na Salama Zaidi Tanzania, huku Afisa Mtendaji Mkuu wake akitwaa tuzo kadhaa za CEO Bora wa Mwaka wa Afrika,” amesisitiza Prof. Kitila.
 
Fedha zote zilizopatikana kupitia Hati Fungani ya Jamii, zitaelekezwa katika kutoa mikopo nafuu kwenye miradi endelevu, ikiwemo miradi ya nishati mbadala, miradi ya kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira, miradi ya maji, miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, miradi ya wanawake, vijana, elimu, afya, nyumba nafuu na mingine inayoendana na hiyo.
 
Zoezi hili limefanyika mbele ya Mgeni Rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji – Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania – Mhe. David Concar, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) – CPA. Nicodemus Mkama, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE – Mary Mniwasa, pamoja na wawakilishi kutoka International Finance Co-operation, Orbit Securities na taasisi zingine.

No comments:

Post a Comment

Pages