Mkimbiaji mashuhuri kutoka India, Milind Soman (kulia), Balozi wa India anayemaliza muda wake Binaya Srikanta Pradan (katikati), na Makamu wa Rais Riadha Tanzania (RT), William Kallaghe, wakionyesha fulana zitakazotumika The India-Tanzania Friendship Run.
NA TULLO CHAMBO, RT
'SUPER STAR' wa kimataifa kutoka India, Milind Soman, amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio za urafiki kati ya India na Tanzania 'India-Tanzania Friendship Run' zinazotarajiwa kurindima Jumamosi Desemba 30.
Akizungumza na Waandishi wa habari kwenye Ubalozi wa India jijini Dar es Salaam leo Desemba 27, Soman, aliwasihi Watanzania kutumia michezo hususan kukimbia kama sehemu ya kuburudika huku wakijenga afya ya miili yao.
"Ujumbe wangu kwenu, naomba tujenge utamaduni wa kushirikisha ndugu, familia, jamii kufurahia, kusherehekea huku tukijenga afya," alisema Milind ambaye ana ushawishi mkubwa nchini India na kuwaomba Watanzania walianze hilo Jumamosi na Jumapili kwa kujiandisha kushiriki mbio hizo zitakazoanzia viwanja vya Farasi 'Green Park Grounds' Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo zitakuwa na Kilomita 5, Kilomita 10 na zile ndefu maarufu kama 'Ultra Marathon' Kilomita 120 kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani na kurejea Dar es Salaam, ambazo ndizo Soman atashiriki.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT/AT), William Kallaghe, alisema wamefarijika kushirikishwa na Serikali zote mbili, Tanzania na India, katika tukio hilo la kihistoria.
"Kwa ujio wa tukio hili tuna promote Ultra Marathon nchini, tunazipongeza Serikali zote mbili kwa kufanikisha tukio hili ambalo linaimarisha ushirikiano wa Tanzania na India na kuhamasisha mchezo wetu wa Riadha," alisema Kallaghe na kuongeza.
Haya ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Saluhu Hassan nchini India Oktoba mwaka huu na ana matumaini dirisha zaidi la ushirikiano kwa tukio hilo kuwa endelevu na nafasi ya wanariadha kwenda India na India kuja Tanzania, pia ni sehemu ya kutangaza vivutio vya utalii nchini.
Naye aliwasisitiza washiriki kujitokeza kwa wingi kujisajili kushiriki mbio hizo, ambapo usajili ni bure kabisa.
Alibainisha kuwa, ratiba inaanza saa 11 alfajiri Jumamosi kwa mbio za Kilomita 5 na 10, kisha Milind Soman akiungana na wanariadha wengine wa Tanzania wataanza ile mbio ndefu Dar- Bagamoyo Kilomita 60 ambako watapumzika na kesho yake Jumapili watarejea tena viwanja vya Farasi jijini Dar es Salaam Kilomita 60, kutakapokuwa na sherehe kubwa ikipambwa na Msanii Darasa.
Milindi Soman, katika maisha yake ameshiriki marathon zaidi ya 100, amewahi kuwa mshindi wa mashindano ya kuogelea kwa miaka minne nchini India, ni mwanamitindo, mtu wa mazoezi ya viungo na mcheza filamu.
Mbali na kufanikiwa kuishawishi familia yake, mke, watoto wake na mama yake mzazi kushiriki mbio, ana ushawishi mkubwa nchini kwa jamii kuishi kwa utamaduni wa kufanya mazoezi ili kujenga utimamu wa mwili.
No comments:
Post a Comment