HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 29, 2023

Waziri Silaa awapiga Marufuku Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji kujihusisha Uuzaji Viwanja

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa ameagiza Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji kote nchini kutojihusisha na mauzo ya viwanja na vipande vya ardhi.

Aidha ameweka wazi kuwa watakaohusika ni maofisa ardhi kwa kushirikiana na kampuni za upangaji na upimaji wa ardhi kwenye maeneo na miji husika huku akipiga marufuku wananchi kutonunua maeneo ya ardhi ambayo hayajapimwa au kupangwa na Serikali.

Waziri Silaa ameyasema hayo alipokuwa akitoa  tathmini ya siku 100 za utekelezaji tangu alipoteuliwa kushika wadhifa wa Waziri mwenye dhamana na masuala ya ardhi kupitia mkutano wa Jukwaa la Wahariri (TEF) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

"Kwa wale wanaokwenda kununua viwanja vijijini hakikisha umeitishwa mkutano wa kijiji kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa uamuzi wa kupewa ardhi na ikiwezekana tumia simu kurekodi kwa kukubaliwa kupewa hilo eneo," amesema Silaa.

Waziri Silaa amewasisitiza Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa kuwa wana kazi ya kusimamia watumishi walio chini yao kwa kujipanga vizuri na wana uwezo kubadilisha jinsi sekta ya ardhi inavyoendeshwa nchini kote.

 

Waziri Silaa ameongeza kuwa Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wanachapa kazi vizuri katika mikoa yote, utendaji kazi wao utafanya taswira ya Wizara iende mbele kutekeleza maelekezo ya viongozi wa kifaifa na kuleta tija kwa watanzania.

 

Aidha, Waziri Silaa amesema wizara yake itaendelea kushirikiana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na wataendelea kupokea na kuheshimu ushauri wanaoutoa kuhusu shughuli za sekta ya ardhi nchini.

 

Awali akimkaribisha Waziri kwenye kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga amesema kuwa Menejimenti ya Wizara na taasisi zilizochini ya Wizara kwa kushirikiana na Makamishna Wasaidiza wa mikoa wapo tayari kupokea maelekezo ya Mhe. Waziri kwa kuwa ndiye mwongoza njia ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi katika sekta ya Ardhi.

 

Waziri Silaa ametimiza siku 100 katika nafasi hiyo ambayo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Agosti 30, 2023 na kuapishwa Septemba 01, 2023.



No comments:

Post a Comment

Pages