HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 27, 2023

Mtandao wapongeza zuio la kuingiza mbegu

Na Mwandishi Wetu

 

MTANDAO na Muungano wa Mashirika ya Kiraia na Vikundi vya Wakulima vinayounda Kikosi Kazi cha Mbegu Tanzania wamepongeza uamuzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), kuzuia ingizaji mbegu za mahindi na maharage ya Soya kutoka nchini Malawi.


 

Pongezi hizo zimetolewa mtandao huo, kupitia Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Mbegu cha Tanzania, Abdallah Mkindi ambapo amesema dhamira yao ni kutetea  haki na ustawi wa wakulima wadogo katika sekta ya mbegu. 

 

Alisema kikosi hicho kinalenga kuendeleza mifumo ya mbegu inayosimamiwa na wakulima, ambayo inategemea kanuni za kilimo ikolojia, bioanuai, na uhuru wa chakula.

 

“Sisi wanachama wa Kikosi Kazi cha Mbegu cha Tanzania, tunatoa pongezi zetu za dhati kwa juhudi za zilizochukuliwa na Wizara ya Kilimo na TPHPA kwa kuhakikisha maslahi ya wakulima wa Kitanzania na uadilifu wa mfumo wetu wa mbegu na kilimo cha kitaifa,” alisema.

 

Alisema wanapongeza uamuzi wa kishujaa wa kuzuia uagizaji wa mbegu za mahindi kutoka Malawi, kwani ni hatua muhimu katika kulinda wakulima na watumiaji kutokana na hatari inayoweza kuhusiana na mbegu zilizobadilishwa vinasaba kwa njia ya Uhandisi Jeni  (GMOs). 

 

“Uamuzi wa kuchukua hatua haraka kufuatia ripoti juu ya uwezekano wa kuwepo vinasaba vya GMO unaonyesha dhamira ya kuhakikisha usalama na anuai ya mfumo wetu wa mbegu wa kitaifa,” aliongeza.

 

Alisema pia wanatambua marufuku ya kuagiza soya na bidhaa zake kutoka Malawi na kwamba uamuzi huo, uliozingatia uchambuzi wa hatari za wadudu, unadhihirisha kwamba walikuwa wanaenda kinyume na azma ya TPHPA ya kuhifadhi anuai ya kilimo na kulinda wakulima wa Kitanzania kutokana na tishio la madhara yanayoweza kusababaishwa na Virusi vya Tobacco Ringspot (TRSV).

 

Mkindi alisema wakati wakiunga mkono jitihada hizo, wanaiomba Wizara ya Kilimo, inayosimamia majukumu ya wakala wake ikiwa ni pamoja na TPHPA, kuhamasisha marekebisho ya Sheria ya Mbegu (2003) ili kutambua na kulinda mbegu zinazosimamiwa na wakulima.

 

Aidha alisema wanahimiza TPHPA kusukuma kwa haraka kupitisha Mkataba wa Kimataifa wa Rasilimali za Jenetiki za Mimea kwa Chakula na Kilimo (ITPGRFA) kwa kutoa Sheria ya Kitaifa ya Rasilimali za Jenetiki za Mimea (NPGR) kwa matumizi rasmi na ya mamlaka, kwani itasaidia katika usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za jenetiki za mimea.

 

“Tunahimiza serikali kuimarisha kanuni za tahadhari kwa kudumisha utimilifu wa Sheria za Usalama wa Bioteknolojia. Uangalizi wa kina kwenye mipaka ni muhimu kuzuia kuingia kwa mbegu zisizostahili ambazo zinaweza kuhatarisha mfumo wetu wa kilimo,” alisema.

 

Mwenyekiti huyo aliyataja mashirika ambayo yapo kwenye kikosi kazi kuwa ni Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO), Iles de Paix (IDP), PELUM Tanzania, Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM), Sustainable Agriculture Tanzania (SAT), ECHO EA, ESAFF, AfroNET, ENVIROCARE na MVIWAARUSHA.

 

Mengine ni MVIWAKI, MVIWAMA, TUSHIRIKI, ACTIONAID Tanzania, SWISSAID Tanzania, HACHAWOTA, SHIWAKUTA na COWEA.

No comments:

Post a Comment

Pages