Mkurugenzi wa Wateja Wadogo
Benki ya CRDB, Boniventure Paul (wa pili kushoto) akimkabidhi mfano wa
tiketi ya ndege mshindi wa Kampeni ya Benki ya CRDB ‘Tisha na Tembocard
Tukakiwashe AFCON’ Evelyne Rwebugisa, katika hafla iliyofanyika Makao
Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam leo Disemba 22, 2023. Wa pili
kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Kadi CRDB, Farid Seif.
Na Francis Dande, Dar es Salaam
BENKI ya CRDB kwa kushirikiana na
kampuni ya Visa inayoongoza katika mfumo wa malipo ya kidigitali,
imekabidhi tiketi kwa mshindi wa kampeni ya ‘Tisha na Tembocard Tukakiwashe AFCON’.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya tiketi ya ndege kwa mshindi wa Kampeni hiyo, Evelyne Rwebugisa, jijini Dar es Salaam leo Disemba 22, 2023, Mkuu wa Kitengo cha Kadi Benki ya CRDB, Farid Seif amesema kuwa lengo la kampeni hii ni
kuhamasisha matumizi ya kadi zake za TemboCard Visa, ambapo wateja
nane watakaofanya miamala mingi zaidi watapelekwa nchini Ivory Coast
kushuhudia mashindano ya TotalEnergies CAF Africa Cup of Nations (AFCON)
2024.
Kampeni
hiyo ambayo ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na Benki ya CRDB kupunguza
matumizi ya fedha taslimu na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya
kidigitali ilizinduliwa Novemba 2, 2023 na itadumu kwa
miezi mitatu mpaka Januari mwakani.
Mshindi wa kampeni hiyo Evelyne Rwebugisa amesema "Nimefurahi sana na sikutegemea kabisa, nachoweza kuwaambia wateja wengine wazidi kutumia kadi, wazidi kuchanja uwezi jua labda kadi yako ndio safari yako"
Evelyne ameongeza kuwa ushindi huo umetokana na kufanya malipo kwa kutumia kadi badala ya fedha taslimu katika manunuzi mbalimbali ndani na nje ya nchini.
Washindi
wa kampeni hii watalipiwa nauli ya safari yao ya kwenda Abidjan, malazi
katika hoteli ya kifahari, tiketi za daraja la juu (VIP) za kushuhudia
mchezo wa fainali, kuhudhuria matukio maalum na vingine vingi ambavyo vitawaachia kumbukumbu isiyofutika.
Mbali
na kushinda safari hiyo, wateja watakuwa na fursa ya kushinda zawadi
nyingine ikiwemo seti ya sofa na vifaa vya kielektroniki mfano runinga
na friji. Ili kushinda, amesema wateja wanaweza kutumia kadi zao kulipia
bidhaa wanapozinunua dukani au sokoni, kwenye vituo vya mafuta,
hotelini, wanaponunua tikiti au kulipia huduma.
No comments:
Post a Comment