HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 10, 2023

Wanne wafariki katika ajali ya gari Kagera

 Na Lydia Lugakila, Bukoba

Watu wanne wamefariki  dunia huku wengine 21 wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha gari lenye usajili namba T 339 DBV aina ya Hiace  iliyokuwa ikitokea Izimbya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kuelekea Bukoba Mjini mkoani Kagera.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Blasius Chatanda,wakati akiongea na waandishi wa habari katika eneo la tukio na kusema kuwa ajali hiyo ilitokea majira saa tano na nusu asubuhi maeneo ya Kyetema katikati mwa Kata mbili za Kemendo na Bujugo Halmashauri ya Bukoba.

Kamanda  Chatanda,alisema watu walipoteza maisha ni watu wazima watatu  na mtoto moja huku kati ya majeruhi 21 watoto ni 4 watu wazima 17 ambao walikimbizwa katika hospitali ya Bujuna ngoma ambayo ni ya Wilaya hiyo.

Alisema kutokana hali ya majeruhi  wengi kuwa mbaya wengine wamehamishiwa katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kagera Bukoba kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.

Alisema chanzo cha ajali hiyo uchunguzi wa awali umebaini ni mwendo kasi dereva alipokuwa akishuka kwenye mteremko mkali aliweka gari free (Newtro )hivyo alishindwa kuirudisha kwenye mfumo wa gia  na kugonga nguzo za umeme zilizokuwa kando ya barabara na pikipiki zilizokuwa kwenye maegesho ya barabara.

“Uzembe wa mtu mmoja  unaweza kusababisha kesho waliopata ajali kupata elemavu wa kudumu na kuwa tegemezi katika familia au jamii “alisema Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera.

Hata hivyo kamanda wa Polisi Mkoani humo amewataka madereva  wazingatie sheria za usalama barabarani wanapokuwa wanaendesha vyombo vya  moto na wakiwa na abiria.

Aidha alisema kuwa hadi sasa haijafahamika kama dereva yuko hai au amefariki huku akidai kuwa ikithibitika yuko hai sheria itachukua mkondo wake.

Aliongeza kuwa  waliofariki na majeruhi walio wengi  bado hawajatambuliwa hivyo amewataka Wananchi kufika katika hospitali hizo kutambua ndugu zao.


No comments:

Post a Comment

Pages