HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 10, 2023

Waziri Chana azindua mpango wa usajili wa watoto chini ya miaka 5 Dar


Waziri wa Sheria na Katiba,Balozi Dkt. Pindi Chana akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mpango wa kuanza zoezi la usajili wa watoto chini ya miaka mitano kwa mkoa wa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Watoto zaidi laki mbili wanatarajiwa kusajiliwa mpaka zoezi litakapohitimishwa mapema mwakani.


 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

 

 

Waziri wa Sheria na Katiba,Balozi Dk.Pindi Chana amezindua mpango wa kusajili watoto chini ya miaka mitano Jiji la Dar es Salaam na kuwataka wakazi kujitokeza kwa wingi na kuleta watoto kusajiliwa na kupata vyeti bure.

 

Akizungumza  kwenye sherehe za uzinduzi huo kwenye Viwanja vya Zakhem Mbagala wilayani Temeke mwishoni mwa wiki,Dkt. Chana amesema hiyo ni fursa kwa  wakazi wa Dar es Salaam na vitongoji  vyake kujiokeza na kuchangamkia zoezi hilo linaloratibiwa na Wakala wa Usajili na Udhamini (RITA).

 

‘’Vyeti  vya kuzaliwa vinaumuhimu sana kwa watoto wetu kwakuwa watakapo fika elimu ya juu itawasaidia kuwatambua na kuwaingiza kwenye mifumo mbalimbali na mpango huu umeonekana kuwa na faida kubwa kwa watanzania kwani wameitikia wito huu, na ni wasihi wakazi wa Dar es Salam wajitokeze kwa wingi kwani hili ni agizo kutoka kwa Rais wetu Dkt. Samia suluhu Hassan," Alisema Waziri Chana 

Naye,Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, amesema kuwa chini ya mpango huo RITA inategemea watoto zaidi 200,000 wasajiliwe wakati wa zoezi hili linalolenga kuhakikisha watoto wote wenye miaka chini mitano wanasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa bure.

 

‘’Azma yetu ni kuhakikisha kuwa hadi kufikia mwakani asiwepo mtoto yeyote mwenye kukosa cheti kwani zoezi hili ni mahususi kwa watanzania wote na hakuna gharama yoyote katika zoezi hili pia huduma zetu zitatolewa katika vituo vyote vya afya vilivyo katika ngazi ya mkoa, wilaya hadi kata’’ alisema Bw. Kanyusi.

 

Aidha,Bw. Kanyusi aliongeza kuwa hadi sasa mkoa wa Dar es Salaam umefikia asilimia 60 ya utoaji vyeti kwa watoto na sasa wanakamilisha kwa kuwafikia watoto waliobakia ambapo kwa mujibu wa sensa ya makazi na watu ya mwaka 2022 mkoa wa Dar es Salaam unajumla ya watoto 624,755 ambao kati yao asilimia 60 ndio waliopata vyeti na watoto 248,298 ndio waliopo kwenye mpango huu wa kupewa vyeti bure.

 

Kwa upande wake,Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa  la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke wisch, amesisitiza umuhimu wa watoto kuwa na kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzawali kwani inaisaidia serikali kuweka mipango yake vizuri kuhusiana na suala la watoto.

 

"Tunatambua umuhimu wa watoto kuwa na vyeti ndiyo maana tumejitokeza kuwaunga mkono RITA kwani cheti kitamtambulisha mtoto mahari popote aendapo na hii itarahisisha sana katika kujua taarifa zake muhimu’’ alisema  Bi.  wisch.

 

Naye Mwakilishi kutoka kampuni ya simu za mkono ya TIGO, Rukia Mtingwa mbali ya kuipongeza RITA kwa mafanikio makubwa katika zoezi la usajili watoto amesema kupitia  kampuni yake ambayo huduma zake zipo nchi nzima naimesaidia kufanya zoezi kuwa rahisi.

 

"Sisi kama tigo tumetambua umuhimu wa hili jambo hivo tumekuja kuwaunga mkono RITA kwa kuhakikisha TEHAMA inasaidia kurahisisha utekelezaji wa mpango huu, hivo tumehakikisha kuwa mtu yeyote anafikiwa na huduma hii kwa simu ya mkononi mahali popote alipo’’ alisema Bi. Mtingwa.

 

Tangu mpango huo uzinduliwe umeshatekelezwa katika mikoa 25 na watoto zaidi ya milioni nane wameshasajiliwa na kupata vyeti bure ambapo mpango utahitimishwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na watoto zaidi ya laki mbili wanarajiwa kusajiliwa.


 

No comments:

Post a Comment

Pages