Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama akikabidhiwa mfano wa hundi ya shilingi za kitanzania milioni 47 na Makamu Mwenyekiti wa Wanajumuiya wa Kampuni za Kuongoza Uwindaji wa Kitalii Tanzania (Tanzania Hunting Operators Association-TAHOA), Abdulkadir Mohamed kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa nyumba za waathirika wa maafa ya Hanang, leo Januari 4,2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam . Wanaoshuhudia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (wa tatu kutoka kulia), Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi (wa pili kutoka kushoto) na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa, Katibu wa TAHOA, Suleiman Masato (wa pili kutoka kulia) na Katibu Mtendaji wa TAHOA, Erasmus Tarimo (kulia).
NA MWANDISHI WETU
Jumuiya ya Kampuni za Uwindaji wa Kitalii Tanzania (Tanzania Hunting Operators Association-TAHOA) imetoa salamu za pole jamii ya Wana Hanang waliopatwa na maafa yaliyosababishwa na maporomoko ya tope na mawe kutoka mlima Hanang mkoani Manyara na kusababisha vifo, majeruhi, uharibifu mkubwa wa miundombinu na mali.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo hii leo Januari 04, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa JNCC Jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa TAHOA, Abdulkadir Mohamed amesema kuwa michango waliotoa ni michango iliyotolewa na makampuni ya uwindaji kwa namna walivyoguswa na ni kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi wa nyumba za waathirika wa maafa hayo.
Alieleza kuwa, umoja huo umechanga fedha za kununua vifaa vya ujenzi vyenye gharama ya shilingi shilingi za Kitanzania milioni 47,409,800 ambavyo vitapelekwa Hanang.
“Sisi kwa umoja wetu tumechanga fedha za ununuzi wa vifaa vya ujenzi ambavyo vitapelekwa Hanang hivyo tumeungana na Serikali kwa kuamua kukabidhi mchango wetu utakaosaidia wananchi wa Katesh Hanang kurejesha hali zao za maisha katika ubora zaidi,” alisema Abdulkadir
Akitoa neno la Shukrani mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama aliishukuru kampuni ya TAHOA kwa namna walivyojitoa kuungana na Serikali na kazi kubwa iliyofika huku akisema kuwa kazi kubwa iliyopo ni kurejesha hali hasa makazi kwa wana Hanang.
“Mmekuja wakati sahihi kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo ni vifaa vya ujenzi, hivyo mmeleta msaada huu utasaidia vitu muhimu vinavyohitajika kwa ujenzi ikiwemo saruji ambayo itasaidia kupata makazi salama na sahihi kwa Wana Hanang”, alieleza Mhe. Mhagama.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amewashukuru TAHOA kwa kuonesha utayari wao wa kuweza kuchanga kwa ajili ya waathirika wa maafa ya Hanang huku akieleza kuwa zoezi lote limefanikiwa kutokana na uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuungana na watanzania waliofikwa na maafa hayo.
“Kipekee nikupongeze Waziri mwenye dhamana ya uratibu, Mhe. Mhagama kwa namna umelisimamia hili na kuhakikisha hali za wakazi wa Hanang zinarejea, hakika mmefanya kazi kubwa sana kwa maeleklezo ya Mheshimiwa Rais wetu,” alisisitiza Waziri Kairuki
Umoja wa Jumuiya ya TAHOA unajumuisha wanachama kutoka kampuni za Robin Hurt Safaris Ltd, Tanzania Big Game Safari Ltd, Tanzania Safaris and Hunting Ltd, Safari Royal Holding Ltd,EBN Hunting Safaris Ltd, African Buffulo Safaris Tracers, Michel Mantheakis Safaris Ltd, Luke Samaras Safaris Ltd, Pori Trackers of Africa Ltd, Bushman Safaris Trackers Ltd, Game Frontiers of Tanzania Ltd, Rungwa Game Safaris Tanzania, Eshkesh Safari Ltd, Mwatisi Safaris Ltd, Ilaroi Ranching Ltd, Tanzania Game Trackers Safari Ltd na Transports Costings.
No comments:
Post a Comment