Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, akifungua Mafunzo ya kuwajengea uwezo Wawezeshaji na Walimu wa
shule binafsi, waweze kuikabili vema mitaala iliyoboreshwa,
yaliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na kufanyika katika
Ukumbi wa Shule ya Msingi Bernard Bendel, Kola B mjini Morogoro, leo
Januari 2, 2024.
Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Mitaala TET Dk. Fika Mwakabungu, akimkaribisha Katibu Mtendaji wa TAPIE Laurent Gama kutoa neno la shukurani.
Katibu Mtendaji wa TAPIE Laurent Gama akitoa neno la shukurani.Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa 'wamefurika' ukumbini.
Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia imemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa yanayoendelea
katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa miundombinu lengo likiwa
kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu iliyo bora.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, wakati
akifungua Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Wawezeshaji na Walimu wa
shule binafsi, waweze kuikabili vema mitaala iliyoboreshwa,
yaliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na kufanyika katika
Ukumbi wa Shule ya Msingi Bernard Bendel, Kola B mjini Morogoro, leo
Januari 2, 2024.
Kuhusu mafunzo hayo Prof. Carolyne alisema
Serikali imeidhinisha Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la
Mwaka 2023 pamoja na Mitaala iliyoboreshwa ya mwaka 2023, hivyo
kuidhinishwa kwa mitaala kumeleta uhitaji wa mafunzo kwa wasimamizi na
watekelezaji wote wa mitaala hiyo.
Alisema, mifano mbalimbali
duniani inaonesha ujenzi wa mfumo bora wa elimu unategemea kwa kiasi
kikubwa ubora wa walimu wanaouendesha hivyo ni wazi ili mabadiliko
yoyote ya sera na mitaala ya elimu yaweze kuleta tija iliyokusudiwa ni
lazima walimu waandaliwe vema.
"Aidha, ili mitaala itekelezwe kwa
ufanisi, ni lazima kuwe na walimu wenye weledi, maadili na ari stahiki,
kwa kulitambua hili, Serikali imejipanga kutoa mafunzo ya walimu kazini
kwa walimu wote wa shule za umma na zisizo za Serikali ili kuwawezesha
kuielewa mitaala iliyoboreshwa na kuitekeleza kwa ufanisi", alisema
Prof. Carolyne.
Alisema mafunzo hayo yatasimamiwa na TET ambayo
tayari imeandaa wawezeshaji wa kitaifa wakiwemo wahadhiri kutoka katika
vyuo vikuu vya umma na binafsi, Wakufunzi wa Vyuo vya Serikali na
visivyo vya Serikali, Wathibiti Ubora wa Shule na Maafisa Elimu Kata na
hadi sasa wawezeshaji 10,557 wa Kitaifa wameshawezeshwa kuweza kutoa
mafunzo husika katika maeneo zilizopo shule zote.
"Kutokana na
uhitaji mkubwa wa mafunzo na idadi kubwa ya walimu inayohitaji
kuwezeshwa, Serikali kupitia TET imeona ni vyema kuongeza namba ya
wawezeshaji wa kitaifa kutoka katika kundi la shule zisizo za Serikali
na hili ni moja ya makubaliano ya kikao kati ya Serikali na viongozi wa
taasisi mama zinazosimamia shule zisizokuwa za serikali (umbrella
organisations) kilichofanyika Disemba 29, 2023.
Nimejulishwa kuwa
katika kikao chenu mlikubaliana kuwa taasisi mama zitaletawashiriki
mahiri kumi watakaowezeshwa na TET na kuwa washiriki hawa watasaidia
kwenda kujenga uwezo kwa walimu wengine wa shule zisizo za Serikali, ni
kwa msingi huo pia TET imeona ni vema itumie fursa hiyo pia kuwawezesha
walimu wote wa shule zisizo za Serikali katika Manispaa ya Morogoro", "
alisema Prof. Carolyne.
Prof. Carolyne alizipongeza taasisi mama
kwa kukubali kushirikiana na Serikali katika kuongeza idadi ya
wawezeshaji watakaoendelea kutoa mafunzo haya kwa walimu na kuwashukuru
pia kwa kuwagharamia washiriki kutoka katika taasisi hizo na kuwezesha
upatikanaji wa eneo linalotolea mafunzo hayo.
Pia aliwapongeza
washiriki waliohudhuria mafunzo hayo, akisema ana matumaini kuwa
watatumia fursa hiyo muhimu kushiriki kikamilifu kwa muda wote wa
mafunzo kwa ajili ya kujiandaa vyema kutekeleza mitaala kwa umahiri na
kufanikisha lengo la Serikali la kuboresha elimu nchini.
"Ninapenda
kusisitiza kuwa mafunzo kwa walimu wa shule zisizo za Serikali
yasiendeshwe kama biashara kwa kuwalipisha walimu. Wawezeshaji kutoka
shule zisizo za Serikali mtawezeshwa kama nilivyosema, lakini
hamtaruhusiwa kwenda kufanya biashara ya mafunzo kwa walimu juu ya
utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa.
Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia na OR-TAMISEMI kupitia Wathibiti Ubora wa Shule na Maafisa
Elimu Kata watafuatilia kuhakikisha kuwa walimu wa shule zisizo za
Serikali hawatozwi fedha za mafunzo, ili kuhakikisha mafunzo haya
hayachangishwi, Serikali kupitia Wizara itatoa mwongozo utakaoweka
bayana kuwa mafunzo haya ni bure kwa walimu wote na kuwa mwalimu
hatatozwa chochote," alisema Prof. Carolyne.
Ili kufanikisha
hilo, Prof. Carolyne. aliiagiza TET kuendelea kufanya uratibu wa mafunzo
yote yanayohusu utekelezaji wa mitaala kwa kushirikiana na taasisi mama
za shule zisizo za Serikali, na kamwe mawakala wasitumike katika
kuratibu au kutoa mafunzo hayo.
Alisema, Ili kuhakikisha Serikali
inapata taarifa na ufuatiliaji wa mafunzo hayo anaielekeza TET kuratibu
mpango mzima wa utoaji wa mafunzo, kukusanya takwimu zote muhimu na
kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mafunzo.
"Naomba pia
kusisitiza kuwa sualala Mafunzo ya Walimu Kazini ni la lazima na siyo
hiari kwa walimu wote nchini wa shule za umma na shule zisizo za
Serikali, hivyo, hata baada ya mafunzo haya tuendelee kujenga umahiri wa
walimu kwa kupitia utaratibu wa mafunzo endelevu ya walimu kazini yaani
MEWAKA.
Kwa kuzingatia umuhimu wa mafunzo haya, nimatarajio
yangu kuwa wote mnaoshiriki mafunzo haya mtayafuatilia kwa umakini ili
yalete matokeo chanya katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, kwa
kufanya hivyo mtakuwa mmesaidia kuiwezesha Serikali kufikia azma yake ya
kuleta mabadiliko ya kweli katika mfumo wa elimu nchini", alisema Prof.
Carolyne.
TET
Mapema akimkaribisha Katibu Mkuu,
Mkurugenzi Mkuu wa TET Dk. Aneth Komba alisema utoaji wa mafunzo hayo
umefanyika kufuatia kukamilika kwa kazi ya uboreshaji wa mitaala ya
elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu ambako kumeleta uhitaji wa
kuwawezesha walimu kufahamu maboresho yaliyofanyika ili waweze
kutekeleza tendo la ujifunzaji na ufundishaji kwa kadiri ya matarajio ya
mitaala.
Alisema, mafunzo hayo yaliyoanza leo yatatolewa kwa
siku tatu kwa makundi mawili ya wawezeshaji na walimu wa Darasa la Awali
na Elimu ya Msingi wanaofundisha shule zisizo za serikali na kwa idadi
yatahusisha wawezeshaji 163 na walimu 600 jumla ni 763.
Dk. Aneth
alisema lengo kuu la Mafunzo kwa wawezeshaji ni kuongeza idadi ya
wawezeshaji wa Kitaifa smbao watashirikiana na TET katika kutoa mafunzo
kwa walimu wote wa darasa la Kwanza mpaka la Sita. Kwa hiyo baada ya
mafunzo haya inataraajiwa kutakuwa na wawezeshaji wengi kutoka shule za
serikali na sisizo za serikali.
"Aidha, lengo la mafunzo kwa walimu wa Darasa la Awali na Elimu ya Msingi ni kuwawezesha kuhusu mambo
mbalimbali
ikiwemo maboresho mahsusi ya mitaala yaliyofanyika ambapo washiriki
watapitishwa katika Muundo wa Elimu, Dira na malengo makuu ya Elimu
nchini, Malengo ya Elimu ya Awali na Msingi, Maeneo ya Ujifunzaji,
umahiri na masomo katika ngazi ya elimu ya awali na msingi mtawalia.
Kwa Mfano maeneo ya ujifunzaji ya Elimu ya Awali yameboreshwa na sasa ni matano kama ifuatavyo:
•Utamaduni,
Elimu ya Imani, Sanaa na Michezo, • Lugha na Mawasiliano, • Stadi za
awali za maisha, • Afya na Mazingira, • Stadi za awali za Kihisabati,
Kisayansi na TEHAMA.
Aidha, maeneo ya ujifunzaji kwa Elimu ya
Msingi Darasa la Kwanza na la Pili nayo yameboreshwa na sasa ni matatu
ambayo ni Lugha, mawasiliano na stadi za hisabati, Utamaduni, Imani
Sanaa na michezo pamoja na Afya na Mazingira", alisema Dk. Aneth na
kuongeza;
"Kwa upande wa Darasa la 1-6 maeneo ya ujifunzaji ni
matano ambayo ni Lugha na mawasiliano, Hisabati, Sayansi ya Jamii,
Sayansi na Teknolojia na Sanaa na Michezo".
Dk. Aneth alifafanua
kuwa, maeneo hayo katika ngazi ya Elimu ya Msingi Darasa la 1- 6
yamebeba masomo ya Kiswahili, Kiingereza lugha za kigeni za Kiarabu,
Kichina na Kifaransa, Hisabati, Historia ya Tanzania na Maadili,
Jiografia na Mazingira, elimu ya Dini, Sayansi na Sanaa na Michezo.
Alimwambia
Katibu Mkuu kwamba Washiriki pia watachambua Mtaala wa elimu ya Awali
na Msingi pamoja na Muhtasari wake kuwawezesha kujifunza juu ya
utekelezaji wa mitaala katika ngazi ya darasa.
"Mfano watapitishwa juu ya muda wa utekelezaji wa mtaala kuanzia muda wa kipindi mpaka
saa
na siku ambazo zinatakiwa katika kutekeleza mtaala kwa mwaka na kwa
ngazi husika. Kwa mfano mtaala wa elimu ya awali unasema kuwa Mwaka wa
masomo una siku 194 sawa na wiki 39 zenye mihula miwili ya masomo.
Muda
wa ujifunzaji kwa siku ni saa tatu na nusu na muda wa kipindi ni dakika
ishirini. Hivyo mtaala unabainsiha muda wa Vipindi vya masomo na muda
wa kufanya shughuli nyingine za ujifunzaji ikiwemo kucheza, kujisomea na
kupumzika", alifafanua Dk. Aneth.
Alisema pia washiriki
watapitishwa katika mambo kadhaa ikiwemo (i) Namna ya Kuchopeka matumizi
ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji wa kila umahiri na masomo,
(ii) Kutumia teknolojia na kufaragua zana katika ufundishaji na
ujifunzaji. (iii) Kuchopeka masuala mtambuaka mbalimbali katika Masomo
Bebezi.
Alitaja baadhi ta Masuala mtambuka yaliyochopekwa katika ngazi ya Elimu ya Awali na msingi kua ni;
Mazingira,
Afya, Elimu jumuishi, Elimu ya jinsia, Elimu ya ya Amani na maadili,
Haki na wajibu wa mtoto, Haki za binadamu, Ulinzi na usalama, Usalama
barabarani, Elimu ya fedha, Elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na
Ushirika na masuala ya muungano.
Dk. Aneth alisema, baada ya
mafunzo hayo kwa wawezeshaji kukamilika jukumu la taasisi mama litakuwa
kuratibu uaandaaji wa mafunzo kwa walimu wa shule zao katika ngazi za
mikoa, Kanda au Halmashauri na zitatoa ratiba ya mafunzo hayo kwa TET
itakayobainisha tarehe, ukumbi na muda wa mafunzo husika ili kuiwezesha
TET kuratibu na kusimamia utoaji wa mafunzo hayo.
"Na jambo hili ni mojawapo ya makubaliano yaliyotolewa katika kikao kati ya serikali na taasisi hizi. Hivyo
TET
itasubiri ratiba husika na tumejipanga kusimamia na kuhakikisha kuwa
mafunzo ya mtaala ulioboreshwa yanawafikia walimu wote wa shule za Umma
na Binafsi na yanawawezesha kutekeleza mitaala kwa usahihi.
Taasisi
zilizotoa washiriki wa mafunzo hayo ni Shirikisho la Wamiliki na
Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Tume ya
Kikristu ya Huduma za Jamii Tanzania (CSC), Baraza Kuu la Waislam
Tanzania (BAKWATA), Tanzania Association of Private Investors (TAPIE),
Baraza la Sunnah Tanzania (BASUTA), Mrtandao wa Elimu Tanzania (TENMET).
Nyingine
ni Tanzania Association of Women Owners of School and Colleges
(TAWOSCO), Umoja wa Wazazi wa CCM Tanzania, Tanzania School Empowerment
and Service Organiation (TASESO), Shule za Wasabato na Shule za Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ).
No comments:
Post a Comment