HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 15, 2024

WASHINDI KILIMANJARO MARATHON WAONYESHWA VIWANJA VYAO KIGAMBONI



Mratibu Maudhui ya Kimtandao RT, Tullo Chambo (wa pili kulia), akiwa na wanariadha Sara Ramadhani na Aloyce Simbu, kwenye viwanja vyao walivyozawadiwa baada ya kushinda mbio za Kili Marathon 2023. Kushoto ni ofisa kutoka kampuni ya Surveyed Plots, iliyotoa viwanja hivyo, Buyuni Kigamboni, Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu


WANARIADHA wa Tanzania waliofanya vizuri kwenye mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon msimu wa 2023 zilizofanyika mjini Moshi Kilimanjaro, wameonyeshwa zawadi zao za viwanja.


Mbali na zawadi za fedha taslimu kwa washindi, waandaaji Kilimanjaro Marathon Company na waratibu Executive Solution kwa kushirikiana na wadhamini wenza, Kampuni ya Surveyed Plots ya jijini Dar es Salaam, waliahidi bonasi ya Mtanzania atakayefanya vizuri kwa upande wa wanaume na wanawake, ikiwa ni motisha ya kuwafanya wafanye vizuri zaidi.


Wanariadha hao ni Sara Ramadhani Makera na Aloyce Felix Simbu, ambapo Simbu ikiwa ni mara ya pili kupata zawadi hiyo, kwani 2022 alifanikiwa kuibuka mshindi katika mbio za Km. 42 na kupata zawadi hiyo.


Sara na Aloyce ambaye ni mdogo


wa Mwanariadha nyota nchini, Alphonce Simbu, walionyeshwa viwanja vyao vilivyoko eneo la Buyuni, Kigamboni jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, zoezi lililoendeshwa na maofisa wa Surveyed Plots Company na kushuhudiwa na Mratibu wa Maudhui ya Kimtandao wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Tullo Chambo.


Baada ya kuonyeshwa viwanja hivyo, zoezi litakalofuata ni ukabidhiwaji wa hati.


Wakizungumza baada ya kuviona viwanja hivyo, wanariadha hao mbali na kushukuru na kupongeza, walisema jambo hilo limekuwa likiwaongezea morali ya kufanya vizuri, na kuwaomba kampuni ya Surveyed Plots kuendelea kuwashika mkono wanariadha wa Kitanzania. 


Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2024, zinatarajiwa kufanyika February 25 kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na usajili wa washiriki unaendelea.

No comments:

Post a Comment

Pages