HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 22, 2024

BBT yazidi kukonga mioyo ya Watanzania

Na Mwandishi Wetu, Njombe

 

WADAU mbalimbali kutoka sekta za kilimo, mifugo na uvuvi wamepongeza utekelezaji wa mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kama  njia itakayosaidia kuzinua sekta hizo kupitia kundi la vijana.

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, mkoani Njombe,  mkulima wa parachichi Fredinand Kivua amesema serikali  kupitia wizara za kilimo, mifugo na uvuvi wamekuja na mpango ambao  kama utasimamiwa vizuri utekelezaji wake mchango wake utaweka alama kwa uhakika wa chakula  na kuinua  vipato sambamba  na kukuza uchumi.

 

“Ninaamini sisi kama wananchi tunapaswa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kupititia wizara za kilimo, mifugo na uvuvi katika kuvutia vijana kujikita katika sekta hizo,”amesema Kivua.

 

Naye Magreth Lwangili amesema utekelezaji  wa mpango  wowote na hasa kipindi cha mwanzo watu  huwa wanakosoa sana na kukaa pembeni kuona kama utafanikiwa lakini mafanikio yanapoonekana  huanza kujisogeza na kujiweka sehemu ya mafanikio  hayo.

 

Amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo ambao umeonesha kuwavutia  vijana wengi kuwekeza na kufanya shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi kwani wanategemea kutengeneza maisha yao na kupunguza  umaskini katika jamii ya kitanzania.

 

“Sisi kama wadau wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) tunaunga mkono  hatua ya serikali ya Awamu ya Sita chini Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuja na BBT  kwani tunaamini vijana wengi  wamevutiwa  na mpango  huo unaolemga kuleta mageuzi katika sekta husika,” amesema Lwangili.

 

Kwa upande wake Razack Sanga, mkulima wa mahindi  Wilaya ya Makete, amesema  mpango huo umekuwa na mchango mkubwa  katika kuwaongezea maarifa vijana juu ya  kilimo biashara, na hivyo  kuwaandaa kuja  kushiriki kikamilifu katika  kuchangia  kukuza pato la taifa.

 

“Tunamshukuru  Rais wetu kupitia  wizara zake  kwa kutoa fursa hii  adhimu  kwa vijana wetu kwani wamekuwa  wakipatiwa  mafunzo ya kilimo biashara, ufugaji wa kisasa na bora samaki utakaochochea  uzalishaji,” amesema Sanga.

 

Tangu mpango BBT uzinduliwe na  Rais Samia mwaka jana Jijini Dodoma,  mwitikio wa vijana kujiunga katika mpango huo ni mkubwa  na hivyo kuongeza matumaini  ya dhamira ya Tanzania  kulisha  Bara la Afrika na dunia kwa  ujumla.

 

Mpango huo unalenga kuwezesha ushiriki wa vijana kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi  na kuhakikisha  unakuwa endelevu utakao changia  kuboresha na kuinua  maisha ya watanzania sambamba na  kutengeneza ajira milioni tatu za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja ifikapo mwaka 2030.

No comments:

Post a Comment

Pages