NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka amegawa doti za sare 125 za vitenge kwa ajili ya sherehe za maadhimisho ya siku ya Mwanamke Duniani zilizogharimu kiasi cha shilingi milioni 2.
Sare hizo ambazo zimegawiwa katikka makundi mbali mbali ikiwemo Jumuiya ya wazazi, Wajumbe wa Baraza la UWT Kibaha Mjini, Wajumbe Wanawake wa Baraza la Wazazi la Wilaya, Wajumbe wanawake wa Baraza la UVCCM Kibaha Mjini Pamoja na Wajumbe Wanawake wa Halmashauri kuu ya CCM Wilaya Kibaha Mjini.
Akikabidhi sare hizo kwa niaba ya Mama Selina Koka Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mji Method Mselewa amesema huu ni Utaratibu wa Ofisi ya Mbunge kupitia kwa Mama Koka kugawa sare kwa wanawake kila mwaka na kila zinapofika Sherehe hizo pamoja na Makongamano mbalimbali.
Kwa Upande wake Mama Selina Koka akizungumza katika mahojiano maalumu kwa njia ya simu alisema kwamba ameamua kutoa sare hizo kwa lengo la kuungana na wanawake wenzake katika kusherekea kwa pamoja siku hiyo.
"Nimetoa sare zipatazo 125 kwa ajili ya makundi mbali mbali ya wanawake,ikiwemo kundi la Uwt,Uvccm,Wazazi,pamoja na chama chenyewe cha Ccm ambapo wao ndio watawakilisha wanawake wengine wote wa Jimbo la Kibaha mjini,"alisema Selina Koka.
Mama Koka alisema kwamba amekuwa akishirikiana bega kwa bega na wanawake wenzake katika mambo mbali mbali ya kijamii ambayo yamekuwa yakifanyika ikiwemo hili la kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Pia aliahidi kuendelea kushirikiana kwa dhati na wanawake wenzake na kuwatakia kila la kheri katika sherehe hizo ambazo kiwilaya zinatarajiiwa kufanyika machi 5 mwaka huu mjini Kibaha.
Pia Mama Koka alifafanua kwamba ameamua kutumia jumuiya hizo ikiwa kama wawakilishi wa wanawake wengine wote wa Jimbo zima la Kibaha mjini kwani sio rahisi kwa kila mmoja kupata sare hiyo kwa ajili ya sherehe hizo.
Katika hatua nyingine amesema kwamba anawapenda wanawake wote na kwamba wajitokeze kwa wingi siku hiyo kwa ajili ya kusherekea siku yao ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuonana na kubadilishana mawazo.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha Mjini Elina Mgonja amemshukuru kwa dhati Mama Koka pamoja na Mbunge kwa kujali wanawake wa Kibaha na kwamba tunapaswa kumtia moyo.
Mgonja alisema kwamba wanawake wa Kibaha wamepata Mama ambaye amekuwa ni mstari wa mbele katika kusaidia mambo mbali mbali ya kijamii pamoja hivyo anastahili sifa na kumthamini.
"Kwa kweli tumefarijika sana kupokea sare hizi za vitenge kiukweli mama Selina koka ni mfano wa kuigwa kutokana na kuonyesha mashirikiano na mahusiano mema katika kila jambo,"alisema Mgonja.
Aidha Mwenyekiti Mgonja alisema kwamba Mama koka amekuwa ni kichocheo kikubwa katika kila nyanja ikiwepo sambamba na kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mitaji na fedha.
Naye Katibu wa UWT Cecilia Ndalu amesema kuwa kitendo cha Mama Koka kujali wanawake ni kitendo cha kipekee sana kwani kuwa mke wa Mbunge hawajibik kwa wanawake moja kwa moja lkn amejigusa na kujali sana.
Wajumbe wengi waliopokea sare hizo wameendelea kuishukuru familia ya Mhe Koka kwa kujitoa na wameahidi kuendelea kumuunga mkono Mhe Koka katika kuhakikisha shughuli zake za utekelezaji wa ilani zinaenda vyema.
Sherehe za Mwanamke zinaadhimishwa Duniani kote na kwa upande wa Kibaha Mjini kilele kitakuwa siku ya tarehe 05/03/2024 katika viwanja vya Mailimoja.
No comments:
Post a Comment