HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 09, 2024

RAIS DKT SAMIA SULUHU HASSANI MGENI RASMI MAADHISHO YA MIAKA 85 YA KANISA LA TAG

Na Magrethy Katengu, Dar es Salaam

 

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 85 ya Kanisa la Tanzania Assemblie of God TAG yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Juni 14 jijini Dar es Salaam.


Hayo yamebainishwa  Mei  8, 2024 jijini Dar es Salaam na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Mchungaji Dkt Barnabas Mtokambali na kuweka wazi kuwa dhima kuu ya maadhimisho hayo ni kumshukuru Mungu kwa uaminifu wake na kuwawezesha kubaki imara kama kanisa, taasisi kwa miaka 85.



Hata hivyo amesema  kuwa maadhimisho hayo yanayotajiwa kuudhuriwa na wageni kutoka nje ya nchi wapatao 200, pia yanalenga kurithisha kwa kizazi kijacho imani ya kipentekoste kwa kuangalia namna watangulizi wao walivyotembea na Mungu na namna alivyowatunza na kutenda mambo ya ajabu.



“Hii itawawezesha kupokea kijiti na kumwishia Mungu katika zama hizi na zijazoili aendelee kutenda makuu, pia kanisa la TAG limekuwa kielelezo cha ujenzi wa umoja, amani na upendo na kutoa huduma kwa jamii,” amesema.



  Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 85 wamefanikiwa kueneza injili ya kristo kwa njia ya mbalimbali ikilenga kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu na jamii kwa ujumla na kuongeza idadi ya washirika nchini kote.


Pia katika kipindi cha miaka 85 wamefanikiwa kujenga vyuo tisa vya theolojia na kuwa na uongozi wenye matawi 71 nchini kote jambo lililosaidia kuwekeza katika mafunzo, uongozi na kusaidia kukuza viongozi wa leo na kesho.



Aidha wamefanikiwa kutekeleza agizo kuu na kuwezesha  wamisionari wa hapa nchini wanaokwenda kutumika katika nchi mbalimbali ikiwemo, Madagascar, Msumbiji, Malawi,Zambia, Congo DRC, Burundi, Uganda, Kenya na Rwanda.Pia wachungaji na watumishi wamekuwa wakitumika katika kuhubir na kufundisha Neno la Mungu nchini kote.



Ameongeza kuwa katika maadhimisho hayo wamejipanga kuwa na ibada kubwa ya kumshukuru Mungu pamoja na kuandaa shughuli kadhaa zinazolenga kuhamasisha jamii kuhimiza umoja na mshikamano huku pia wamejipanga kufanya makongamano  ya vijana zaidi ya 10,000 wenye umri chini ya miaka 34.



Pia wamejipanga kufanya semina maalumu ya uongozi kwa viongozi wa ngazi za juu wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama. Aidha anaishukuru Serikali kwa kuwapa ushirikiano tangu enzi ya Hayati Mwalimu Nyerere hadi sasa katika awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan


No comments:

Post a Comment

Pages