HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 24, 2024

SITAKI KUONA WANAFUNZI WANAKAA CHINI KWA KUKOSA MADAWATI : RC SINGIDA,

Serikali ya mkoa wa Singida amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri Saba za mkoa huo kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa haraka kwenye shule za msingi na sekondari ili kujua hali ya uhaba wa madawati ilivyo na kuchukua hatua ya kuondoa tatizo la wanafunzi kujisomea wakiwa wamekaa sakafuni haraka iwezekanavyo.

Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego ametoa kauli hiyo leo Mei 24, 2024 wakati akizungumza na Viongozi wa Manispaa ya Singida na Walimu wa shule ya Msingi Bomani iliyopo Manispaa ya Singida baada ya kufanya ziara ya kustukiza kwenye shule hiyo kufutia kusambaa kwa picha mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha wanafunzi wa shule hiyo wakifanya mtihani yao wakiwa wamekaa chini.

Halima Dendego amesema picha hizo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimesababisha taharuki kubwa kwa jamii  tofauti na hali ilivyo kwenye shule hiyo ambayo inaupungugu wa madawati Nane.

Ameonya kuhusu tabia ya baadhi ya watu kuchukua picha na kusambaza bila kutafuta ukweli jambo ambalo amesema sio zuri na ni lazima likomeshwe.

Mkuu huyo wa mkoa wa Singida pia ametoa siku Saba kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida kuhakikisha anapeleka madawati Nane yanayohitajika kwenye shule hiyo ili wanafunzi wa shule hiyo ya Bomani waweze kujifunza na kujisomea katika hali bora na nzuri zaidi.

“Serikali imewekeza fedha nyingi katika uboreshaji wa elimu nchini vitu kama hivi wanapotokea vimeleta mstuko mkubwa sio kwa wazazi hata kwa Jamii nzima kwa ujumla jambo ambalo halileti picha nzuri na lazima likomeshwe” Amesisitiza Halima Dendego.

Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bomani JOACHIM MSECHU amesema sio kweli kuwa shule hiyo inaupungufu mkubwa wa madawati na upungufu uliopo ni madawati Nane tu na walikuwa kwenye mchakato wa kukarabati madawati mengine yaliyoharibika ili wanafunzi waweze kuyatumia.

 

 

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Singida Godwin Gondwe amemhakikishia Mkuu wa mkoa wa Singida kuwa maelekezo aliyoyatoa watayafanyia kazi kuanzia sasa ili kuondoa mapungufu madogo madogo yanayotokea kwenye sekta ya elimu ili kuimarisha shughuli za ufundishaji wa wanafunzi mashuleni.

Kwa sasa shule ya msingi Bomani iliyopo katika Manispaa ya Singida ina wanafunzi 894 na walimu 16.

 

Imetolewa na

Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya

Mkuu wa mkoa wa Singida.

0755 516 591

0712 762 097.

PTC – 1. Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza kwenye Kikao na Walimu pamoja na Watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida katika shule ya msingi Bomani.

PTC – 2 Watendaji wa Manispaa ya Singida wakisikiliza maelekezo ya Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego kuhusu namna ya kuondoa tatizo la uhaba wa madawani mashuleni.

PTC 3---5 Wanafunzi wa Shule ya Msingi Bomani katika Manispaa ya Singida wakiwa darasani wanajisomea.

PTC 6--- 8 . Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza na Wanafunzi wa shule ya Msingi Bomani mara baada ya kufanya ziara ya kustukiza shuleni hapo ili kujua hali halisi ya wanafunzi kukosa madawati.

PTC – 9 . Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Singida Godwin Gondwe mara baada ya kumaliza kikao na Walimu wa shule ya msingi Bomani na Watendaji wa Manispaa ya Singida.

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages