HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 22, 2024

Wavunaji Kahawa mbichi na Wafanya Magendo Wilayani Kyerwa watangaziwa kiama

Na Lydia Lugakila, Kyerwa

Serikali Wilayani Kyerwa Mkoani Kagera imeahidi kula sahani moja na baadhi ya Wananchi watakaojihusisha na Biashara ya Magendo ya Kahawa na uvunaji wa Kahawa mbichi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mussa Jumanne Afisa Tarafa Mabira kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa wakati akitoa maelekezo ya Serikali katika kikao cha Baraza la Madiwani kilicholenga kujadili taarifa ya utekelezaji wa robo ya tatu kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2023/2024.

Jumanne alisema kuwa Serikali Wilayani humo imejipanga kisawa sawa kuhakikisha inaweka uimara zaidi maeneo ya mipakani ili kuzuia  Kahawa kuvuka kwenda nje ya Nchi na Kupambana na wavunaji Kahawa mbichi kwani jambo hilo husababisha  kuikosesha mapato Halmashauri.

Aliongeza kuwa ulinzi wa kutosha utaanzia mipakani na endapo Wananchi wa aina hiyo wakibainika watachuliwa hatua za kisheria huku akitoa tahadhari mapema kwa wale wenye nia isiyo njema ya kuacha mara moja tabia kuvusha Kahawa kwenda nje ya Nchi.

"Kwa namna ambavyo Mwaka Jana tulidhibiti Kahawa uwenda mwaka huu ikawa mara mbili yake Serikali tumeendelea kujipanga na kamati ya usalama ya Wilaya pamoja na timu ya Magendo kuhakikisha Kahawa haivuki kwenda nje ya Nchi" alisema Jumanne.

Aliongeza kuwa Wakati huu wa kuelekea msimu wa Kahawa na kama Kahawa ilivyo zao muhimu katika Wilaya hiyo kupitia Baraza hilo Wananchi wanatakiwa wavune Kahawa iliyokomaa vinginevyo watakaoshindana na vyombo vya Serikali kukiona cha moto

"Kumekuwepo tabia ya baadhi ya Wananchi wasio na dhamira njema na Serikali kwa kulenga kuikosesha mapato Halmashauri pia naelekeza Halmashauri na wataalam wake kuendelea kubana kwenye ukusanyaji wa Mapato kutokana na kuwepo na maduka mengi mtaani ambayo hayana leseni kabisa" alisema kiongozi huyo.

Aidha alimuelekeza Afisa Biashara wa Wilaya hiyo kuhakikisha anazunguka kila kichochoro ili kutoacha mianya mingi ya ukusanyaji wa mapato ambapo alisasisitiza Watumishi wa Halmashauri hiyo kuendelee kukusanya mapato ili Halmashauri hiyo iendelee kuimarika

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Bahati Henerco alisema kuwa mfumo uliotengenezwa kwa mwaka uliopita kwa kushirikiana na vyombo vya Wilaya juu ya kudhibiti Magendo vilisaidia sana  hivyo hoja ya Kahawa zinavuka haipaswi kusikika masikioni bali ikemewe huku nguvu ya pamoja ikihitajika ili kuepuka kuuza bidhaa nje ya bila utaratibu.

Hata hivyo baadhi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo akiwemo Bi Devotha Biashara ambaye ni Diwani viti maalum kata ya Itera Tarafa ya Nkwenda alisema kuwa wao kama Madiwani watahakikisha Biashara ya Magendo inakomeshwa huku akiwaomba Wananchi kutovuna Kahawa mbichi kwani kwa kufanya hivyo ni kupoteza uhalisia na ubora wa zao hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages