HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 11, 2024

Vijana UVCCM Kagera wataka Mwenyekiti UVCCM ajiuzulu

Ni kwa kauli yake ya kupoteza wanaotukana mitandaoni
 

Na Mwandishi Wetu, Kagera

VIJANA wa Chama cha Mapinduzi  Mkoa wa Kagera wamemtaka Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa huo Faris Buruhan kuomba radhi au kujiuzulu kwenye nafasi yake kwa matamshi yake ya hivi karibuni kutaka kuwapoteza watu wanaotukana viongozi mitandaoni.
 
Faris alitoa kauli hiyo hivi karibuni akiwa kwenye ziara katika Mji mdogo wa Rulenge Wilayani ya Ngara mkoani Kagera.
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo  mkoani hapa, kijana ambaye ni kada wa chama hicho Mohamed Ismail, alisema kauli hiyo imewashangaza watu wengi na isipochukuliwa hatua watu wabaya wanaweza kuitumia kuichafua serikali ambayo haikumtuma kusema maneno hayo.

Alisema vijana wa mkoa huo wanasikitishwa na kauli iliyotolewa na mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa huo na kwamba wanalaani kauli hiyo inayoleta taswira mbaya na kuwaweka kwenye wakati mgumu vijana wa chama hicho.


Alisema kauli ya Mwenyekiti huyo imekiuka  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 77 inayompa kila mtu haki ya kuishi na kwamba ingawa wanapinga watu wanaotukana mitandaoni lakini si kusara kusema atawapoteza.

Kada mwingine wa chama hicho, Innocent John, alisema hata Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi alikemea kauli hiyo mara tu alipoitoa lakini wanamshangaaa mwenyewe kutojitokeza na kuomba radhi hadharani ingawa muda umepita.

 “Dk. Nchimbi akiwa mikoa ya kusini alikemea kauli hiyo akisema kuwa ni ya kijinga lakini mwenyewe amekaa kimyaaa kwa hiyo sisi tulitarajia baada ya kauli ya Dk. Nchimbi ambaye ndiye mtendaji mkuu wa chama, Buruhan angejitokeza na kuombaa radhi lakini amekaa kimya tu hali inayoonyesha dharau sasa hii itatuletea shida sisi vijana, “ alisema John

“Tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025 sasa anapozungumza Mwenyekiti wa UVCCM Kagera inaonekana hilo jambo linatuwakilisha sisi wote kwa hiyo lazima ajitokeze aombe radhi akishindwa ajiuzulu,” alisema

“Kwa maslahi mapana ya nchi yetu tunamwomba ajiuzulu kama ameshindwa kuomba radhi kwasababu ilemeta taharuki na itatusumbua sisi kwenye chama,” alisema

Kijana mwingine wa UVCCM, Ibrahm Rweyongeza alisema moja ya kanuni za maadili ya chama hicho inasema kazi ya kiongozi wa chama ni kulinda chama, kukijenga na kukilinda, kuwa na maadili na kutotenda maovu na kuwa na maadili na kutimiza wajibu wake.

“Ibara ya tano ya Kanuni za UVCCM inasema kazi ya umoja huo ni kulinda na kujenga ujamaa, ujamaa tunaujua unasema watu wote ni sawa hakuna mwenye mamlaka ya kumpoteza mtu yeyote kwa hiyo tunaona mwenzetu amekwenda kinyume na maadili ya chama chetu,” alisema Rweyongeza

“Sisi vijana tunaomba Buruhan ajitokeze hadharani aombe radhi laakini kama atashindwa kufanya hivyo aachie ngazi kwasababu si kwamba anatuharibia sisi wanaCCM mkoa wa Kagera tu anaharibia vijana wa nchi nzima. Kazi ya UVCCM ni kupika viongozi na viongozi wenye maadili mema siyo wa aina hii,” alisema

Alisema Dk. Nchimbi aliwahi kuwa  Mwenyekiti wa UVCCM kwa muda mrefu na alifanyakazi zake kwa uadilifu hali ambayo imewavutia viongozi kumpa nafasi mbalimbali za uongozi na sasa Katibu Mkuu wa chama hicho hivyo wanataka kuona vijana wanafuata mfano wa Dk. Nchimbi.

No comments:

Post a Comment

Pages