HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 31, 2024

WAKURUGENZI MADAI YA WALIMU SIO SIRI YAWEKENI WAZI-Dkt. Msonde

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde akiwa na wanafunzi wa shule ya Sekondari Kashozi alipowasili shuleni hapo kwa ajili ya kufanya kikao kazi na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.

 

Na James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI

 

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amesema, madai ya walimu yanayotokana na uhamisho na likizo sio siri na kuwataka Wakurugenzi  wa Halmashauri zote nchini kuweka wazi orodha ya wanaodai na utaratibu wa malipo ya madai hayo ili kuondoa dhana potofu ya uwepo wa upendeleo pindi yanapolipwa na Serikali.

 

Dkt. Msonde ametoa wito huo kwa wakurugenzi wote wa halmashauri nchini, wakati wa vikao kazi vyake na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na Manispaa ya Bukoba.

 

“Wakurugenzi Madai ya walimu sio siri, yawekeni wazi ili mwalimu ajione ni wa ngapi katika orodha ya malipo na anadai kiasi gani,” Dkt. Msonde amesisitiza.

 

Dkt. Msonde amewataka Wakurugenzi pindi wanapowalipa walimu kupitia fedha za serikali kuu au mapato ya ndani, waweke wazi kiasi kilichopo na kitawalipa walimu wangapi kwenye orodha ya wanaodai, na kuongeza kuwa kila fedha inayopokelewa kwa ajili ya kulipa wanaodai iwekwe wazi ni kiasi gani kimepokelewa na kitaweza kuwalipa walimu wangapi.

 

Sanjari na hilo, Dkt. Msonde amezitaka Halmashauri kutohamisha watumishi kama hakuna ulazima na hakuna pesa za kugharamia uhamisho wa watumishi ili kuondokana na madeni yanayoepukika.

 

“Hamisheni walimu iwapo kuna ulazima unaotokana na ujenzi wa shule mpya, na kwakuwa shule mpya zinajengwa kutokana na mipango inayotekelezwa hivyo fedha kwa ajili ya uhamisho wa walimu zinapaswa kuwa zilitengwa pia,” Dkt. Msonde amehimiza.

 

Dkt. Msonde amehitimisha siku ya pili ya ziara yake mkoani Kagera ambapo amefanikiwa kufanya vikao kazi na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba pamoja na Manispaa ya Bukoba ambayo inalalamikiwa kwa kutowalipa walimu stahiki zao za uhamisho na likizo ya mwaka.

No comments:

Post a Comment

Pages