HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 28, 2024

MISA-TAN yaomba kupunguza ada leseni mitandao ya kijamii

Mwandishi Wetu

TAASISI ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN), imeiomba serikali kupunguza viwango vya ada ya kuendesha mitandao ya kijamii (Blogs, Online Tv na YouTube ili kuvutia vijana kumiliki mitandao kisheria na kujiajiri.

Aidha MISA-TAN imeomba serikali kuharakisha kuunda baraza huru la habari na mfuko wa kusaidia wanahabari nchini kujiendeleza kielimu.

Ombi hilo limetolewa na Mjumbe wa Bodi ya MISA-TAN, Mussa Juma  leo June 26, jijini Dar es Salaam, wakati akifunga warsha ya siku moja kwa wanachama zaidi ya 33 wa taasisi hiyo na waandishi waandishi wengine kutoka katika vyombo vya habari.

Warsha hiyo iliandaliwa na MISA-Tan kwa ushirikiano na Shirika la Protection International Afrika na kudhamiwa na  Serikali ya Finland.

Juma amesema, gharama ya sh 500,000 ya leseni ua kumiliki blogs na millioni moja kumiliki luninga za mtandaoni ni kubwa kwa vijana na watu wenye ulemavu.

"Kama ada ya leseni ikiwa ndogo vijana wengi wenye taaluma ya habari na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), watamiliki mitandao ya kijamii kisheria na kutoa habari" amesema.

Amesema kwa sasa kutokana gharama kubwa za leseni karibu robo tatu ya mitandao inaendeshwa  bila leseni .

Amesema muhimu serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kugawa mitandao ya jamii ambayo inamilikiwa kibiashara na ambayo inafanya kazi ya kutoa elimu na kupashanahabari pekee.

Juma  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA) na Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanahabari ya MAIPAC, pia ameomba serikali kuharakisha kuudwa baraza huru la habari, bodi ya ithibati na mfuko wa kusaidia wanahabari.

Akizungumza kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Msaidizi wa Maelezo, Patrick Kipangula amesema serikali kupitia TCRA bado inaendelea na utafiti juu ya masuala ya leseni na ada mbalimbali na wakikamilisha watatoa taarifa.

Kipangula hata hivyo aliwataka wanahabari na wadau wa habari kuheshimu sheria na kanuni za masuala ya habari .

Awali wakitoa mada katika warsha hiyo, Mawakili Gedion Mandes , Ofisa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Raymond Kanegene na Deus  Kibamba walitaka wanahabari kusoma kanuni za maudhui ya mitandaoni ili kutovunja sheria.

Wakili Mandes licha ya kushauri kupunguzwa ada za leseni alitaka elimu zaidi kutolewa juu ya kanuni hizo na kuzingatia haki za makundi ya walemavu.

Naye Wakili Kanegene akichambua kanuni hizo amesema zinamapungufu lakini lazima kwa sasa zifuatw.

Alibainisha baadhi ya mapungufu kanuni kukataza kuandika habari za kuchochea biashara ya kamari mitandaoni huku serikali ikipokea kodi.

Kwa upande wake Kibamba amesema lengo la kanuni za maudhui mtandaoni ni kudhibiti usambazaji holela wa habari na taarifa.

"Katika kanuni hii kuna mambo mazuri na mabaya hivyo ni muhimu kuzijua kanuni, ili wakati ukitaka kuzipinga uwe na uelewa," amesema.

Akizungumza katika kongamano hilo Mkurugenzi wa MISA-TAN, Elizabeth Riziki amesema taasisi hiyo itatumia njia ya majadiliano na serikali na wadau katika kudai kanuni nzuri za maudhui ya mitandaoni lakini pia sheria bora.

Amesema anaishukuru serikali ya awamu ya sita walau imeboresha baadhi ya sheria na kanuni na imefungua milango ya majadiliano zaidi ili kuboresha uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.


No comments:

Post a Comment

Pages