HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 28, 2024

SAGCOT kuinua kilimo cha viazi mviringo

Na Mwandishi Wetu, Songea

KITUO cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kimeulezea Mkoa wa Ruvuma kama ni eneo lenye ardhi nzuri inayofaa zaidi kwa uzalishaji wa kilimo cha viazi mviringo na kuinua maisha ya wakazi mkoani humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Lusitu Agro-Business, Benno Mgaya amesema taasisi yake kwa kushirikiana na SAGCOT walipima udongo maeneo mbalimbali ya Wilaya za Songea, Namtumbo na Halmashauri ya Madaba na kubaini kuwa kuna ardhi nzuri yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha viazi mviringo.


“Kuna maeneo mbalimbali ambayo tumeyaainisha na tayari tumeshaanzisha mashamba darasa kwa mfano shamba letu la kwanza lilikuwa katika Kijiji cha Sirikano, Kata ya Liganga, Wilaya Songea tukianzia mbegu za viazi mviringo tani 100 tu,”amesema Mgaya,

Kwa mujibu wa Mgaya maeneo mengine ambayo mashamba darasa yapo katika Wilaya ya Songeni ni Peramiho, Litapwasi na Namatuhi. Kwa upande Wilaya ya Namtumbo shamba darasa limeanzishwa eneo la Mtyangimbole ambapo kwa Halmashauri ya Madaba lipo Shule ya Tanga Stendi.

“Ubora wa ardhi katika maeneo haya unamwezesha mkulima kupata mazao kati ya tani 20 hadi 25 kwa hekari moja,” amesema na kuengeza kuwa Ruvuma kwa siku za mbeleni utakuwa miongoni mwa mikoa itayoongoza kwa ulishaji wa viazi mviringo.

Amesema zao la viazi linaweza kulimwa katika misimu yote ya mwaka na hivyo kumwezesha mkulima kuwa fedha za kutosha mwaka mzima kwani kilimo cha viazi mviringo kitafanyika wakati wa masika na wa kiangazi kwa kufanya kilimo cha  umwagiliaji.

Akizungumzia kuhusu viazi mviringo, Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT,  Geoffrey Kirenga ambaye ni Bwana shamba mbobezi amesema Ruvuma ipo katika nafasi nzuri ya kuweza kubadilisha maisha ya wananchi endapo watachukulia kilimo cha viazi mviringo kwa uzito wake.

“Kama SAGCOT tupo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa zao la viazi mviringo katika Wilaya Songea linakuwa na mafanikio na kuleta mafanio chanya katika kubadilisha maisha ya wakulima,”  amesema Kirenga.

Utafiti uliofanywa na SAGCOT Wilaya ya Songea kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 umebaini kuwa viazi mviringo vimetoka matokeo mazuri katika uzalishaji ambapo hekari moja inaweza kuingiza hadi zaidi ya Sh milioni 10.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Mjini, Michael Mbano amesema mara ya kwanza aliambiwa kwamba hekari moja ya viazi inawezakulisha gunia 200 za viazi hakuamini mpaka pale alipojioonea mwenyewe.

“Kwa sasa nimeamini pale Mheshimiwa Rais anaposema ajira nyingi zipo shambani ninaungana naye pasipo shaka. Nawashukuru sana SAGCOT na wadau wake kwa kutufungua macho na kutuonyesha fursa iliyojificha,” amesema Meya Mbano.

SAGCOT imekukuwa muhimili mkubwa katika kuchocheo maendeleo ya kilimo biashara kwa kuwaunganisha wakulima wadogo na kati kwa kutoa mafunzo sambamba kuwaunganisha na taasisi za kifedha na masoko ya uhakaki kwa mazao yao.

No comments:

Post a Comment

Pages