NA TULLO CHAMBO, RT
MSIMU wa Kwanza wa Mbio za Msoga Half Marathon 2024, umefanyika kwa mafanikio makubwa huku Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete akifungua milango kwa wanariadha wa Tanzania kujifua Msoga, Chalinze mkoani Pwani.
Katika mbio hizo zilizoshirikisha washiriki zaidi ya 2000, JK alishiriki mbio za Km. 5 sambamba mkewe ambaye ni Mbunge wa Mchinga mkoani Lindi, Salma Kikwete, Mbunge wa Chalinze na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Prof. Adolph Mkenda na viongozi mbalimbali wa kiserikali na kisiasa.
Rais Mstaafu Kikwete, alitoa fursa kwa wanariadha kwenda Msoga kujifua kwa mazoezi na yuko tayari kuwasaidia.
JK alieleza kufurahishwa na mwanzo wa mbio hizo zilizokuwa na lengo la kuchangia afya ya mama na mtoto kwenye hospitali ya Msoga.
Aidha, JK alikoshwa na idadi kubwa ya washiriki na kwamba hakutegemea.
Katika Km. 21 wanawake mshindi aliibuka Sara Ramadhan wa Arusha akitumia saa 1:10:29 na Failuna Matanga 1:12:12 pia wa Arusha huku nafasi ya tatu ikienda kwa Angel John wa Singida saa 1:12:28:73.
Wanaume, mshindi aliibuka Joseph Panga wa JWTZ saa 1:02:06 wa pili Dickson Paulo wa Mwanza saa 1:02:55 wakati Josephat Gisemo wa Polisi Arusha akitumia saa 1:03:30 nafasi ya tatu.
Km. 10 kwa wanawake, kinara aliibuka Elizabeth Ilanda aliyetumia dakika 37:59 akifuatiwa na Sarah Hhiitii dakika 38:07 wote kutoka Arusha huku Warda Shaban wa Singida akikamata nafasi ya tatu dakika 39:25.
Wanaume, Jumanne Mnada wa Arusha alishinda akitumia dakika 31:25 akifuatiwa na Inyasi Sulle dakika 31:41:58 na Marco Silvester nafasi ya tatu 31:53:16 wote wa JWTZ.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, alisema Msoga Half Marathon imeanza kwa mafanikio makubwa katika kutimiza lengo la kusaidia afya ya mama na mtoto na kwamba itakuwa endelevu.
Alisema, Msoga ni kitovu cha Halmashauri ya Chalinze ambako hospitali ya wilaya inajengwa.
"Uwepo wa hospitali hii ndio umechangia kufanyika kwa mbio za Msoga Marathon ambazo zinawakusanya wadau kuchangia huduma ya mama na mtoto hospitalini hapo.
Mratibu wa mbio hizo, Nelson Mrashani kutoka Rhino Sports Talent, alisema muitikio wa washiriki umekuwa mkubwa kwa wakimbiaji msimu huu wa kwanza.
Mrashani, aliwashukuru wadau na wadhamini wote kwa kufanikisha mbio hizo kwa kiwango bora.
Aidha, Mratibu hiyo aliwaomba radhi washiriki kwa changamoto zilizojitokeza na kwamba maoni yote yatafanyiwa kazi kuongeza ufanisi mbio ijayo.
No comments:
Post a Comment