HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 11, 2024

Rais Samia apokea Gawio la Bil. 637, Msajili wa Hazina asema kiasi hakiridhishi


NA MWANDISHI WETU


WAKATI Serikali ikipokea kiasi cha Sh. Bilioni 637.122, kama gawio na michango kutoka Mashirika na Taasisi za Umma, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesisitiza kuwa kiasi hicho sio cha kuridhisha kulingana na Uwekezaji wa Serikali unaofikia Sh. Trilioni 76 katika mashirika hayo.

Kwa mara ya kwanza Serikali imepokea gawio kwa pamoja – hafla iliyofanyika chini ya kaulimbiu; ‘Mageuzi ya Mashirika ya Umma na Wajibu wa Kuchangia Maendeleo ya Tanzania,’ ambapo pia Msajili Mchechu amemuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuridhia uanzishwaji rasmi wa Siku ya Gawio Tanzania.

Aidha, Msajili ameenda mbali kwa kumuomba Rais Samia kuhudhuria kikao kikuu cha kila mwaka cha Wakuu na Wenyeviti wa Bodi wa Taasisi za umma kitakachofanyika Agosti mwaka huu na kwamba ukubwa wa gawio lililotolewa unatokana na kuwepo kwake katika Kikao Maalum cha Agosti 2023.

“Mheshimiwa Rais, mbele yako ni Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa mashirika yasiyopungua 300, kati ya mashirika 304 yanayosimamiwa na Msajili wa Hazina. Kati ya hayo, yale ambayo Serikali tuna asilimia nyingi za umiliki, yapo 248 na yale ambayo tuna hisa chache ni 56.

“Leo unapokea gawio la jumla ya shilingi 637,122,914,887.59, likijumuisha shilingi 278,868,961,122.85 kutoka kwa Mashirika ya Biashara na michango ya shilingi 358,253,953,764.74 kutoka katika taasisi nyingine. Makusanyo haya ni kwa kipindi kinachoanzia Julai 2023 hadi Mei 2024.

“Hata hivyo kwa kuwa Mwaka wa Fedha wa 2023/24 bado haujakamilika, makusanyo bado yanaendelea, na tunatarajia kufikisha kiasi cha Sh. Bil. 850. Hivyo, kupitia hadhara hii, nitoe rai kwa wale ambao wanadaiwa au hawajatoa, kuhakikisha wanakamilisha malipo yao kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha,” alisema.

Mchechu alifafanua kuwa, mashirika yaliyochangia gawio hilo ni 145, ambalo ni ongezeko la mashirika 36 kutoka 109 yaliyochangia mwaka jana na kwamba mashirika 159 hayajachangia kabisa katika Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mwaka huu.

“Idadi hii sio ndogo, hivyo tunatoa wito kuwa taasisi zote zibadilike na kuboresha utendaji wao wa kazi utakaowawezesha kuanza kuchangia ama kuongeza uchangiaji katika Mfuko Mkuu wa Serikali, ambalo kimsingi sio suala la kujitolea au fadhila kwa Serikali, bali ni wajibu wa lazima.

“Kwa kuzingatia Uwekezaji wa Serikali katika mashirika, ambao unafikia Sh. Trilioni 76 hadi sasa, kiasi cha gawio na michango kinachokusanywa hadi sasa sio cha kuridhisha na tunaamini kuwa waliokabidhiwa kuongoza mashirika haya, wanaweza kufanya vizuri zaidi kwa faida ya taifa na wananchi wote kwa ujumla,” alisisitiza.

Alifafanua ya kwamba mwenendo huo sio mzuri sana ikiwa kila mmoja miongoni mwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu anataka kuyafikia malengo aliyoyatoa Rais Samia mwaka jana ya kuhakikisha wanafikia asilimia 10 ya Mapato ya Kikodi, na anaamini kuwa wahusika wote walimuelewa.

“Naamini tulikuelewa vizuri mwaka jana na kuwa tutachukua hatua za dhati kabisa ili kuleta mabadiliko chanya na ya haraka katika mashirika haya na hivyo kusaidia kukuza uchumi wa nchi yetu.

“Ieleweke kuwa, ili kufikia lengo tarajiwa la kuimarisha mchango wa Mashirika ya Umma na Taasisi ambazo kuna Uwekezaji wa Serikali katika kujenga uchumi na maendeleo endelevu ya nchi, basi mabadiliko ya kiusimamizi, kiutendaji na kiuendeshaji hayaepukiki,” alisisitiza Mchechu.


 

No comments:

Post a Comment

Pages