HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 11, 2024

Rais Samia aridhia ombi la kutenga Siku Maalum ya Mashirika ya Umma kutoa Gawio

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akipokea Gawio la Sh. Bilioni 57.3 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dkt. Edwin Mhede (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kulia) wakati wa hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Wakala, Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa, hafla hiyo ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo Juni 11, 2024. (Na Mpiga Picha Wetu).

Rais Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wakati wa hafla ya Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa gawio na michango kwa Serikali iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa gawio na michango kwa Serikali iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Msajili wa Hazina, Thobias Makoba, akizungumza wakati wa hafla ya Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa gawio na michango kwa Serikali iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.



 

 

Na Mwandishi Maalum


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la Msajili wa Hazina Mhe. Nehemia Mchechu la kutenga siku maalum kila mwaka na kuwa siku ya Mashirika na Taasisi za Umma kutoa gawio kwa Serikali.

Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akihutubia kwenye hafla ya Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa gawio na michango kwa Serikali iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

 Aidha, Rais Samia amesema Serikali inaweka mazingira bora ya kufanya biashara, kutunga sera rafiki zinazohamasisha uwekezaji nchini kwa nia ya kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za jamii.

 Vilevile, Rais Samia amesema upokeaji gawio ni ishara kuwa mazingira yaliyowekwa yanafanya kazi na kuwezesha kupatikana kwa fursa ya kufanya biashara na kupata faida. Rais Samia pia ametoa wito kwa viongozi wa Mashirika yote ambayo bado hayajatoa mchango wake kwa Serikali, na yale ambayo yametoa chini ya kiwango wanachotakiwa kutoa, kuhakikisha wanafanya hivyo kabla ya Mwaka wa Fedha wa 2024 haujaisha.

Hali kadhalika, Rais Samia amesema kuwa ataendelea kusimamia mageuzi katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma ili kuyawezesha kujiendesha kibiashara na kwa tija zaidi kwa manufaa ya Watanzania.

Rais Samia ameelekeza Mashirika kufikia mwezi Desemba 2024 kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana kama walivyofanya Shirika la Mapato nchini (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).

Katika hafla hiyo, Rais Samia amepokea gawio na michango kutoka kwa mashirika 145 yenye thamani ya jumla ya Shilingi 637,122,914,887.59 ikijumuisha gawio Shilingi 278,868,961,122.85 kutoka katika Mashirika ya Biashara na michango Shilingi 358,253,953,764.74 kutoka katika Taasisi nyingine.

No comments:

Post a Comment

Pages