HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 12, 2024

Ubadhirifu wa kutisha Msikitini

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini (RITA), imebaini ubadhirifu mkubwa wa kiasi cha shilingi bilioni moja za Kitanzania katika Msikiti wa Ijumaa uliopo Jijini Mwanza na hatua za kisheria zimeshaaza kuchukuliwa.
 

Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani Mwanza  mwishoni mwa wiki, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw Frank Kanyusi aliwaambia waumini wa msikiti huo kuwa ziara yake  ili lenga  kuwasilisha ripoti ya ubadhirifu wa fedha  kwa waumini  sambamba na kusimamia uchaguzi wa  wasimamizi  watakao simamia kwa muda mali za waumini wa msikiti.

“Rai yangu kwa wajumbe wa Bodi  ya Udhamini  wahakikishe  wanatekeleza majukumu yao  kama Sheria inavyowaelekeza au kuwataka na waelewe kuwa wao siyo wamiliki  wa  mali  bali ni wasimamizi  wa mali kwa niaba ya  wanachama  hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuzuia vitendo visivyofaa,” amesema Kanyusi.

Kwa mujibu wa Kabidhi Wasii Mkuu huyu, Februari 2 mwaka huu mwaka huu aliunda  Kamati ya Uchunguzi ambayo ilifanya kazi kwa kipindi cha mwezi mmoja   na ikaja na ripoti iliyoonyesha ubadhirifu wa fedha takribani shilingi bilioni moja za msikiti,

“Hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa  sambamba na wale wote waliohusika kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria. RITA imewatoa hofu waumini wote kuwa mali zote za waumini wa msikiti zipo kwenye mikono salama,” amesema.

Kufuatia ubadhirifu na mivutano miongoni mwa baadhi ya waumini, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma ilielekeza iundwe kamati ya wasimamizi  kabla ya Juni 20 mwaka huu, itakayosimamia mali zote za waumini wa Msikiti wa Ijumaa Mwanza.

Kwa upande wake, Afisa Sheria wa RITA, Emmanuela Mwingira amesema RITA imeshafanyia kazi marekebisho ya Katiba na kuchagua waumini kadhaa wa msikiti huo watakaofanya uchaguzi ili kupata bodi ya wadhamini.

“Kazi tuliyokuwa nayo  ni pamoja na kupitia sheria yao  na kufanya maboresho ili  kuzuia makosa  kutojirudia siku za mbeleni,” amesema   Mwingira na kupongeza utulivu na ushirikiano uliotolewa wakati wote wa kikao na waumini wa msikiti.

Naye Muumini wa   Msikiti huo, Sherally Sherally amesema sheria isipofuatwa haki  haitopatikana na  kuiomba RITA kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika na ubadhirifu wanachukuliwa hatua stahihiki pamoja na kufikishwa mahakama.

Tukiendelea kuwachekea watu wanaojilimbikizia mali za waumini hatutafika mbali sambamba hilo pia wale tutakaowachagua watafanya hivyo hivyo kwani watajua hakuna tutakachowafanya,” amesema Sherally na kuiomba serikali kupitia mahakama kuchukua hatua kali za kisheria na kutoa fundisho kwa wengine.

Muumini huyo, alionyesha imani yake  kwa serikali  ya  awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassani katika kushughulikia na kutatua kero na changamoto zilizowasilishwa kwa kufanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi wa kudunu.

Muumini mwingine Abdallah Tawfique mbali ya kuipongeza RITA hatua iliyozichukua, aliishukukuru pia serikali ya awamu ya sita kwa kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa taasisi zote za dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini.

Bodi ya kwanza ya udhamini ya msikiti huo ilivunjwa na serikali mwaka 2020 na baadaye kuundwa  kwa Kamati ya mpito ya wajumbe kumi na watatu ambayo nayo imevunjwa na Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma kufuatia mvutano wa baadhi ya waumini uliokuwa unaendelea.



No comments:

Post a Comment

Pages