HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 12, 2024

Wakulima Chunya waomba kujengewa maghala ya nafaka

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

WAKULIMA wa mazao ya nafaka wilayani Chunya mkoani wa Mbeya wameiomba serikali kuwajengea maghala ya kuhifadhia mazao  ili kuepuka uuzaji holela wa mazao yao kwa wachuuzi kwa bei ya hasara.

Wakizungumza mara baada ya mafunzo ya teknolojia ya kisasa ya kilimo endelevu cha zao la Soya yaliyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na  Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) wamesema kuwa uwepo wa maghala utasaidia uuzaji wa mazao kwa  kuzingatia bei elekezi ya serikali na maslahi ya wakulima.

Zacharia Mwambene ambaye ni  mkulima wa zao la Soya  wilaya hapo   alisema wakulima wengi wamekuwa wakijihusisha na kilimo cha zao la mahindi kwani ardhi waliyonayo inarutuba na inafaa kulima mazao ya nafaka  lakini  kikwazo ni ukosefu  wa maghala ya kuifadhia mazao hayo  hali inayochangia  wakulima kutochangamkia fursa ya zao la soya.

“Serikali yetu inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu natumaini itasikia kilio chetu ikiwa ni pamoja na kujengewa maghala ya kuhifadhia mazao hali itakayo chochea   uzalishaji wa mazao likiwemo zao la soya,” amesisitiza Mwambene.

Kwa upande wake Suzan Silindwe mbali ya kuishukuru serikali kwa kuwajengea uwezo  utakaongeza uzalishaji wa zao la soya hapa nchini na hivyo sekta  lazima serikali izingatie mahitaji ya wakulima sambamba na kujenga maghala pamoja na kuwepo kwa soko ya uhakika wa zao hilo.

“Mafunzo tuliyopata yatasaidia kuleta matokeo chanya katika uzalishaji wa zao la soya wilayani hapa kwani uzalisahji wenye tija na kuchangia pato la mkulima mmoja mmoja na kutoa mchango stahiki kwenye pato la taifa,” amesema Silindwe.

Naye Afisa kilimo Wilaya ya Chunya, Cuthbert Mwinuka alisema halmashauri imeshatenga kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa ghala moja huku wakiendelea na jitihada za kuomba msaada kutoka wizarani kwa ajili ya kuongeza maghala zaidi.

“Sisi kama halmashauri tumetenga ardhi yenye ukubwa wa hekari zaidi ya 50,000 kwa ajili ya kilimo cha zao la soya.  Sambamba na hekari tano kutoka vijiji 23 zitakazo tumika kujenga maghala,” alieleza Mwinuka.

Meneja wa Mpango wa Kilimo endelevu cha soya kutoka SAGCOT, Abdallah Msambachi amesisitiza umuhimu wa kufanya kilimo biashara   na kuwataka wakulima kuanza kufikiria namna bora zaidi ya kuzalisha  katika mnyororo wa thamani katika zao la soya utakuwa na maana kwao.

“Kupitia mafunzo haya waliyoyapata yatawasaidia kufikiria kibiashara  zaidi  na kuondokana na kilimo cha mazoea ambacho hakina tija na matunda yake kwa kile wanachokizalisha yataonekana ,” amesema Msambachi.

Picha kwa Hisani ya UN

No comments:

Post a Comment

Pages