Afisa Kilimo wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Emmanuel Lutego akitoa elimu ya kilimo bora, masoko na fursa zilizopo kwenye Sekta ya Mkonge katika banda la bodi hiyo lililopo kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba).
Na Mwandishi Wetu
MKONGE umetajwa kuwa ni zao ambalo soko lake halitegemei msimu kulinganisha na mazao mengine ambapo mkulima au mfanyabiashara anaweza kuvuna na kuuza wakati wowote katika mwaka.
Akizungumza kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa kilimo wa TSB, Emmanuel Lutego amesema kutokana na hali hiyo, wadau wanaotaka kuingia kwenye sekta ya Mkonge hawatakiwi kuhofia masoko kwamba watauza wapi au wakati gani kwani moja ya jukumu la Bodi ya Mkonge ni kuwaunganisha wakulima na masoko ya mkonge.
Pamoja na mambo mengine amesema; "kama nchi tuna mkakati wa kufikisha tani 120,000 ifikapo 2025 kwa hiyo tunahitaji wakulima zaidi na mashine za uchakataji ili kufikia malengo hayo.”
Aidha, ametaja mikakati ya kufanikisha malengo hayo ni kuongeza ukubwa wa mashamba na idadi ya wakulima wa mkonge kwa kuhamisisha na kutoa elimu ya kilimo bora cha mkonge katika mikoa yote inayofaa kwa kilimo cha mkonge.
“Lakini pia tumejipanga kuongeza tija ya uzalishaji, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mkonge, kuanzisha vituo vya uchakataji wa mkonge(decortication centres) kwa wakulima wadogo,” amesema Lutego.
No comments:
Post a Comment