HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 27, 2024

Mwarobaini kupunguza majanga migodini wapatikana

•  Zege yapigiwa chapuo, magogo kuzuiwa

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini, Tume ya Madini imepata mwarobaini wa kupunguza majanga kwenye migodi kwa kuwaelimisha wachimbaji wadogo kutumia zege kwenye kingo za miamba badala ya magogo.


Akizungumza leo Julai 26, 2024 katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Tume ya Madini kutoka Idara ya Ukaguzi  wa Migodi na Mazingira yaliyofanyika jijini Dodoma, kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Meneja wa Mazingira Mhandisi Ephraim Mushi amesema njia mbadala ya zege kwa wachimbaji wadogo itasaidia kuondoa tatizo la ajali migodini kwa watu kupoteza maisha na wengine kuwa walemavu.

“Wachimbaji wadogo wanatumia magogo maarufu kama matimba kwa kuweka kingo kwenye miamba, sasa njia hii imeonekana sio salama kwa uchimbaji  mdogo kwa maana yanakaa baada ya muda yanaoza, yanaanguka na kusababisha ajali kwenye migodi,”amesema Mhandisi Mushi na kuongeza,
 
“Lakini pia imeonekana wachimbaji wadogo wanatumia sana haya magogo ambayo kimsingi yanaleta uhabiribifu wa mazingira, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini tumeona kuna haja ya kuja na njia mbadala ili kupunguza au kuondoa kabisa ajali migodini.


“Idara ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, elimu hii tutaenda kuitoa kwa wachimbaji wadogo, namna ya kukinga  na zege ili miamba inapoanguka isije kuleta madhara kwa wachimbaji, wakiweza kwenda na huu mfumo uzalishaji utaongezeka na utakuwa na tija na vifo vya wachimbaji vitapungua na mapato ya serikali yataongezeka,”amesisitiza Mushi.


Naye Mjiolojia Mwandamizi Fabian Mshai akitoa shukrani kwa wakufunzi kwa niaba ya washiriki amesema mafunzo waliyoyapata yamejenga   uwezo zaidi, ari na nguvu mpya kwa wakaguzi wa migodi na mazingira katika kutekeleza majukumu yao.


Amesema  kuwa ili uchimbaji wa madini uwe endelevu lazima kuwe na  usalama, kusiwe na ajali na utunzaji wa  mazingira  kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye na ina umuhimu katika kukuza sekta ya madini nchini.

“Elimu hii tutaishusha chini kwa wachimbaji wadogo sambamba na kukagua hali ya usalama mara  kwa mara ili kuwasaidia wachimbaji kuepuka ajali wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.

Mafunzo hayo yalianza rasmi Jumatatu Julai 22 hadi leo Julai 26, 2024  ambapo mawasilisho mbali mbali yaliwasilishwa na wakufunzi   Mhandisi Gervas Wiliam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mhandisi Selemani Msangi kutoka Kampuni ya HETAMIS, Mhandisi Japhet Mmary kutoka Shanta Mining Co. Ltd, Fikiri Juma kutoka Bulyanhulu Gold Mine na  Fey Kidee kutoka Kidee Mining (T) Ltd.


 

No comments:

Post a Comment

Pages