HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 27, 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO LA PILI LA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU UTALII WA VYAKULA VYA ASILI BARANI AFRIKA

Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili akizungumza leo katika ufunguzi wa Kongamano la kwanza la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, Kanda ya Afrika kuhusu Utalii wa vyakula vya asili katika Bara la Africa (Gastronomy) jijini Victoria Falls nchini Zimbabwe.

Rais wa  Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa (katikati) akiwa ameongozana na Mke wake, Dkt. Auxillia Mnangagwa (kushoto) kukagua mabanda ya maonesho ya vyakula vya asili ya kiafrika kwenye Kongamano la kwanza la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, Kanda ya Afrika kuhusu Utalii wa vyakula vya asili katika Bara la Africa (Gastronomy)linaloendelea  jijini Victoria Falls nchini Zimbabwe. Wengine pichani ni Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili, Wake wa Marais wa Serbia, Angola, baadhi ya Mawaziri kutoka nchi za Afrika pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Zimbabwe.

  

Na Mwandishi Wetu- Zimbabwe

 

Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyeji wa Kongamano la Pili la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Kanda ya Afrika kuhusu utalii wa vyakula vya asili katika Bara la Afrika kwa mwaka 2025.

 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili katika ufunguzi wa Kongamano la kwanza la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, Kanda ya Afrika kuhusu Utalii wa vyakula vya asili katika Bara la Africa (Gastronomy) linaloendelea jijini Victoria Falls nchini Zimbabwe leo Julai 27, 2024.

 

Bw. Pololikashvili amemshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Mhe. Angellah Kairuki kwa ushirikiano wake na nia yake ya kutaka kutangaza utalii wa chakula na kusisitiza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani liko tayari kutoa ushirikiano kwa nchi za Afrika katika kutangaza utamaduni wa Kiafrika hasa Utalii wa vyakula.

 

"Afrika sio tu kwa ajili ya safari na kuangalia mazingira ya asili, bali pia tunataka kuuonesha ulimwengu kwamba Afrika ni tajiri katika utamaduni hasa utalii wa vyakula ambao ni sehemu kubwa ya utamaduni wetu" alisisitiza.

 

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kufanyika kwa Kongamano hilo  nchini Tanzania  kutakuwa na manufaa makubwa katika kukuza mnyororo mzima wa thamani katika utalii ikiwemo Utalii wa vyakula hasa kugusa wadau wengi wakiwemo wakulima wafugaji, wavuvi,wazalishaji wa nafaka,wachakataji wa mafuta n.k.

 

"Tunao mwaka mmoja wa kufanya maandalizi na tutajipanga vizuri kuhakikisha kwamba Tanzania inaonesha urithi na utajiri mkubwa tulionao lakini ni nafasi nzuri katika kukuza utalii wetu zaidi" Mhe. Kairuki ameongeza.

 

Amefafanua kuwa kupitia jukwaa hilo kutakuwa na mashindano mbalimbali kwa ajili ya ubunifu  na wenye vyuo na wataalamu wengine watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wenzao kutoka nchi nyingine za Afrika.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Tanzania (NCT), Dkt. Florian Mtey amesema kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania kutakuwa ni fursa kubwa kwao kwani wamekuwa wakitoa mafunzo ya mapishi mbalimbali pamoja na kufanya matamasha ya mapishi kwa nyakati tofauti.

 

Kongamano hilo limefunguliwa rasmi na Rais wa  Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa ambaye amesisitiza juu ya umuhimu wa Sekta ya Kilimo katika kukuza Utalii wa Chakula.


No comments:

Post a Comment

Pages