HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 18, 2024

Serikali yapongeza mafunzo ufundi ya EACOP, CPP kwa vijana wa Kitanzania


Mkuu wa Idara ya VETA  katika chuo cha Ufundi Arusha ( ATC) Mwandisi Seba  Maginga (kulia) akielezea namna wanavyo tumia vifaa vya kisasa kuchomelea kwenye  hafla ya uzinduzi wa programu ya mafunzo inayoitwa   ‘Shielded Metal Arc Welding’ (SMAW),  inayoratibiwa na Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) kupitia mkandalasi wake China Petroleum Pipeline Engineering (CPP) iliyofanyika jana jijini Arusha  wapili kushoto ni  Bi. Neema Kweka Meneja  kitengo cha uwezeshaji kwa wazawa katika mradi wa EACOP.

Meneja  Kitengo cha Uwezeshaji kwa wazawa kutoka Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) Bi. Neema Kweka akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa programu ya mafunzo inayoitwa   ‘Shielded Metal Arc Welding’ (SMAW),  inayoratibiwa EACOP kupitia mkandalasi wake China Petroleum Pipeline Engineering (CPP) iliyofanyika jana jijini Arusha.

Wafanyakazi wa Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP), uongozo wa  chuo cha Ufundi Arusha ( ATC)  wakiwa  Kwenye picha ya pamoja wanafunzi wa programu ya mafunzo inayoitwa   ‘Shielded Metal Arc Welding’ (SMAW),  inayoratibiwa na EACOP kupitia mkandalasi wake China Petroleum Pipeline Engineering (CPP)  mara bada ya  kumalizika kwa afla ya uzinduzi jana jijini Arusha.

 

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Serikali imeupongeza mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) kwa kutoa mafunzo ya uchomeleaji yaani ‘Welding’ kwa vijana 50 kupitia mkandalasi wake China Petroleum Pipeline Engineering (CPP) ili kuwapa fursa ya kazi katika mradi wa bomba hilo.

 Awamu ya kwanza ya mafunzo haya yanayoendelea katika Chuo cha Ufundi Arusha  yanahusisha wanafunzi 25 na awamu ya pili ya mafunzo hayo yatafanyika mwishoni wa mwezi Agosti.

 Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo uliofanyika jijini Arusha jana, Mratibu wa mradi huo kwa upande wa serikali, Asiadi Mrutu kutoka Shirikila la Maendeleo ya Petroli (TPDC) linalomiliki hisa 15 katika mradi huu amesema EACOP kupitia wakandarasi wake mbalimbali imekuwa ikitoa mafunzo na utoaji ajira kwa Watanzania kama sehemu ya uwekezaji wa rasilimali watu kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kimkakati.

 “Kiukweli mradi huu umefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa vya vitendea kazi katika vyuo mbalimbali vya ufundi hapa nchini ili kuwapa mafunzo wanafunzi na walimu wa vyuo hivi  kupitia wataalamu kutoka nje ya nchi,”alisema Bw Mrutu.

 Bw Mrutu alisema lengo la mradi ni kuzalisha wataalamu mbalimbali wazawa ambao watakuja kujiajiri hapo baadaye au kufanya kazi katika miradi mingine ya kimkakati pindi mradi huu wa EACOP utakapomalizika.

 Amesema mradi huo wa EACOP kwa sasa umefikia asilimia 38.2 ya utekelezaji wake na tayari umetoa ajira 4274 kwa Watanzania mpaka sasa kupitia wakandarasi wanaotoa huduma mbalimbali katika mradi huu.

 

Naye Neema Kweka anayesimamia kitengo cha uwezeshaji kwa wazawa katika mradi wa EACOP (Local Content) amesema mradi wa EACOP kupitia kitengo chake unasimamia mambo matatu ambayo ni ajira , uwezeshaji na kutoa kipaumbele cha watoa huduma wa ndani katika kazi katika mradi huo.

 Amesema mradi wa EACOP umekuwa ukiboresha miundombinu ya ufundishaji vyuoni kwa kutumia gharama kubwa ili kuhakikisha nchi inazalisha wataalamu mbalimbali kwa ajili ya kufanya kazi katika mradi huu na mradi mingine ya kimkakati.

 “Tunataka mradi wa EACOP uache alama kubwa sio tu katika kutoa ajira, bali pia kuzalisha wataalamu ambao nchi itajivunia,” amesema wakati wa sherehe za ufunguzi wa mafunzo ya nadharia na vitendo yanayochukua wiki 12 .

Naye Meneja Usimamizi wa Uchumi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) George Kabelwa amesema wakiwa kama wasimamizi wa huduma za nishati hapa nchini, wameipongeza EACOP na CPP kwa mafunzo  yanayoendelea kutolewa na uwekezaji katika vyuo vya ufundi hapa nchini ili kuzalisha wataalamu wa kada mbalimbali ikiwemo kuchomelea.

 Akizungumzia mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kaskazini, Bi Monica Mbelle amesema mamlaka yake inashirikiana na mradi wa EACOP kutoa wataalamu wa ndani wanaoshirikiana na wengine kutoka nje ya nchi.

 Amesema Veta inatoa mafunzo kwa  vijana 147 katika fani mbalimbali ambao wanaweza kufanya kazi katika miradi mikubwa kwa maendeleo ya nchi.

 “Vijana wazingatie vizuri mafunzo haya ambayo yana gharama kubwa sana ili nchi iendelee kuzalisha wataalamu kwa miradi mikubwa kama wa EACOP,” amesema Bi Mbelle na kuishukuru EACOP.

 Naibu Meneja Mradi kutoka CPP, Bw Cai Xiaolong amesema kampuni yake kupitia mafunzo hayo itazalisha watalaamu wenye ujuzi wa kimataifa watakaotumika katika kazi ya uchomeleaji wa bomba la inchi 24 litakalofukiwa kwa kazi ya kusafirisha mafuta ghafi Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.

 Akizungumza kwa niaba ya vijana wenzake, mmoja wa vijana hao Joseph Raphael ameushukuru mradi wa EACOP na CPP kwa mafunzo hayo yatakayowapa ujuzi zaidi na fursa za ajira katika ujenzi wa bomba hilo.

 Bomba hili linapita katika mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga, likijumuisha wilaya 24, kata 134 na vijiji zaidi ya 180.

 Wanahisa wa mradi huu ni TotalEnergies (Asilimia 62), kampuni ya mafuta ya Uganda (UNOC) asilimia 15, CNOOC ya China  asiimia nane pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) asilimia 15.

No comments:

Post a Comment

Pages