HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 08, 2025

Mbeto: ACT haina viongozi wajenga hoja

Na Mwandishi  Wetu, Pemba

Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa  na uwezo mdogo wa kisiasa walionao viongozi  wa ACT  Wazalendo  Zanzibar , tokea kilipompoteza  aliyekuwa Mwenyekiti  wa chama hicho , Marehemu Maalim  Seif Sharrif Hamad.

Vile vile, CCM imekitaja ACT   kimepungukiwa na  viongozi mahiri, wenye uwezo mpana  kisiasa na waliobaki sasa ni wapiga porojo  majukwaani ndio maana hawana Sera wala Ilani inayowaongoza kwenye uchaguzi mkuu 29 Oktoba 2025.


Katibu wa Kamati  Maalum ya NEC  Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis  Mbeto Khamis  aliyesema kwa hilo anawapa pole ACT kwa sasa kwani kinaongozwa kiujanja ujanja.

"Hivi sasa chama hicho kinaongozwa na wanasiasa magube na makanjanja" alidai Mbeto.

Mwenezi huyo alisema chama chochote  makini  cha siasa,   hutangaza sera zake, kutaja dira na mwelekeo ili kichaguliwe, badala yake wamebakiwa na   viongozi walioshindwa kujenga hoja mbele ya umma.

 Alisema  baada ya  viongozi wa ACT kushindwa kuwa wabunifu katika kuendesha   siasa za kisasa,  kimebaki kulitumia jina  Marehemu Maalim Seif huku kikitegemea kupata ushindi wa Urais.

"ACT kimepoteza sifa  baada ya kutokea  kifo cha Maalim Seiif. Hivi sasa kinasubiri majaliwa baada ya kukosa  matarajio. Hiyo ni shida kwa chama kutegemea  uwezo wa mtu mmoja kukipa chama uhai wa kisiasa "alisema.

Alibainisha kuwa chama cha siasa lazima kiwe na misingi na kitengeneze viongozi na sio kuokoteza.

Mbeto alisema chama chao huandaa viongozi toka Chipukizi, Umoja wa Vijana (UVCCM ) na baadae CCM na ndio maana kina hazina kubwa ya viongozi wenye sifa za kuwatumikia wananchi.

  "Ndio maana hata kikifanya mabadiliko ya viongozi  hakipati athari zozote tofauti na ACT au vyama vingine vya upinzani" alisema.

Mbeto ambaye ametaka waZanzibari kumchagua Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa Rais Zanzibar ili amalizie miradi ya maendeleo aliyoianza, alisema kuwa ACT kimepoteza idadi kubwa ya wanasiasa   madhubuti  ambao walifukuzwa CCM na kuhamia CUF enzi hizo.

Wanasiasa hao ambao baadae wakawa ACT ambako wamekutana na kadhia za kiuongozi na kupoteza dira.

"Huko wamekutana na   adha na karaha ya mtu anayeitwa  Ismail Jussa Ladhu matokeo yake wakaletewa figisu chaguzi za ndani ikiwa ni pamoja na ya Urais na matokeo yake ndio yanayoonekana hivi sasa" alisema mwenezi huyo.

Alibainisha kuwa 1987 kundi  la wanasiasa hodari waliotimliwa CCM na kujiunga CUF miongoni mwao waliandaliwa  wakiwa CCM na kukomaa kisiasa. 

"Kwa Siasa za  uzushi na fitna za Ismail Jussa Ladhu, marehemu Maalim Seif Sharriff akafitinishwa na Hamad Rashid Mohamed na upande mwingine Mohamed Dedes na Juma Duni ili mmojawapo asigombee Urais " alisema Mbeto .

Kutokana na hali hiyo ndio maana chama hicho kimepotea na huenda kikasambaratika baada ya 29 Oktoba 2025.



 

 

No comments:

Post a Comment

Pages