HAYAWI hayawi hatimaye yamekuwa, hii ni baada ya Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Silver Strikers yq Malawi na kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL 2025/26).
Katika pambano hilo ndani ya dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Yanga ilihitaji ushindi kama huo ili kutinga hatua ya makundi CAF CL, baada ya wiki Jana kukubali kipigo cha bao 1-0 walipowafuata Silver Strikers kwenye Uwanja wa Bingu Mutharika, jijini Lilongwe.Yanga, ikiongozwa na kocha wa muda raia wa Malawi Patrick Mabedi, ilicheza soka la kasi na kushambulia, hasa katika kipindi cha kwanza ilikofunga mabao yote, shukrani kwa nahodha Dickson Job 'BBD' na kiungo Pacome Zouzoua.
Job alifunga bao lake akiunganisha kona ya Mohamed Doumbia mapema dakika ya Tano, kabla ya Pacome Zouzoua kufunga bao la pili kunako dakika ya 33 ya mchezo huo ambao Yanga iliondoa viingilio na kuruhusu mashabiki kuingia bure.
Tofauti na mechi zote sita ilizocheza msimu huu, leo Yanga imeonesha soka safi la kimbinu, kulinganisha na lile ililoonesha katika mechi tatu za CAF CL, mbili za Ligi Kuu na moja ya Ngao ya Jamii, ambazo timu ilikuwa chini ya Mfaransa Romain Folz, ambaye alitupiwa virago baada ya kuchapwa bao 1-0 walipowafuata Silver Strikers wiki iliyopita.






No comments:
Post a Comment