HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 05, 2026

DC IRINGA AKABIDHI MADAWATI 100 KWA SHULE TANO, ASHUKURU NEW LIFE NA DIWANI SARA PONELA

 NA DENIS MLOWE, IRINGA 


MKUU wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amekabidhi rasmi madawati 100 kwa shule tano za msingi ndani ya Manispaa ya Iringa, baada ya serikali kuyapokea kutoka Kanisa la New Life in Christ kwa ushirikiano na Diwani wa Viti Maalum Kanda ya Kihesa, Sara Ponela.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Wilolesi, DC Sitta alisema msaada huo ni hatua muhimu katika kupunguza uhaba mkubwa wa madawati uliokuwepo katika shule mbalimbali za manispaa.
 “Leo tumekabidhi madawati haya ambayo serikali tumepokea kutoka New Life in Christ wakishirikiana na Diwani wa Viti Maalum Sara Ponela waliguswa na changamoto ya upungufu wa zaidi ya madawati 600 katika Manispaa ya Iringa, wakaamua kuchangia kwa kutengeneza madawati 100,” alisema DC Sitta.


Amesema kanisa hilo lilitafuta mbao, viuma na kutumia mafundi wao kutengeneza madawati hayo, ambayo sasa yamegawiwa kwa shule tano zilizopo katika kata nne tofauti.

 “Huu ni mfano wa kuigwa. Tunatoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo waige moyo huu. Serikali yetu inafanya kazi kubwa ya kujenga shule, hospitali na miundombinu; lakini bado tunahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau,” aliongeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, alisema madawati hayo yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi kukaa wanne katika dawati moja, na kuimarisha mazingira ya kujifunzia.

“Tunawashukuru New Life in Christ na Diwani Sara Ponela kwa kutusaidia madawati 100. Sisi kama serikali tumeongeza jitihada zetu, na tunaahidi kuyatunza madawati haya. Maendeleo ni mchakato serikali hufanya la kwanza, wadau wanaunga mkono,” alisema Mlawa.

Amezitaja shule zilizopokea madawati hayo kuwa ni Wilolesi, Maendeleo, Kigamboni, Kibabwa na Kilongaena.

Mwalimu Mkuu wa Wilolesi, George Kameka, amesema msaada huo umepunguza adha ya wanafunzi kuandika wakiwa wamebanana.
 “Watoto walikaa watatu hadi wanne, na ilileta shida kwenye maandishi yao. Sasa watakaa vizuri na kuandika kwa ufasaha. Tunashukuru sana kwa msaada huu,” alisema.

Shule ya Wilolesi ina jumla ya wanafunzi 1,973, hivyo mahitaji ya madawati yamekuwa makubwa kwa muda mrefu.


Diwani wa Viti Maalum Kanda ya Kihesa, Sara Ponela, ambaye alishirikiana na kanisa hilo kwenye mchakato wa kuchangisha na kutengeneza madawati, alisema waliguswa na changamoto iliyokuwepo shuleni.

 “Tuliona watoto wetu wanakaa chini, tukachukua hatua. Kwa nguvu zetu na sadaka za waumini, tumeweza kutengeneza madawati 100 ambayo yanakaliwa na wanafunzi watatu kila moja tumewaokoa watoto 300 kukaa chini,” alisema.




Amesema kazi hiyo ni mwanzo tu, na wamedhamiria kuendelea kutafuta wadau ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayesoma akiwa amekaa chini.

“Tunataka historia ifike mahali mtoto wa Iringa asisome akiwa amekaa chini. Tutaendelea kutafuta wadau na kuongeza madawati zaidi,” alisema Ponela.


No comments:

Post a Comment

Pages