HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

March 10, 2026

Umoja wa madereva bajaji watoa feni kituo cha polisi Tegeta A

Na Miraji Msala 

Umoja wa madereva wa bajaji katika eneo la Goba Mpakani jijini Dar es Salaam umetoa msaada wa feni kwa Kituo cha Polisi Tegeta A ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani na usalama.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Tegeta A, Nora Gewe, aliwashukuru madereva hao kwa umoja wao na moyo wa kujitolea kusaidia kituo hicho.

Gewe alisema msaada huo unaonesha namna wananchi wanavyoweza kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha uhusiano kati ya polisi na jamii.

Aidha aliwahimiza madereva hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, akieleza kuwa kutokana na kazi yao ya kusafirisha abiria wa aina mbalimbali wana nafasi kubwa ya kubaini viashiria vya uhalifu na kutoa taarifa mapema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa madereva wa bajaji Goba Mpakani ,Magawa Augustino, alisema walichangishana fedha kwa hiari ili kununua feni kama ishara ya kuthamini kazi inayofanywa na Jeshi la Polisi katika kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

Alisema madereva wa bajaji wamekuwa wakifanya kazi bega kwa bega na polisi katika kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama na yenye utulivu, hivyo kuona ni muhimu kuendeleza ushirikiano huo.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Siasa Tegeta A, Marco Vaginga, aliwapongeza vijana hao kwa kujitokeza mara kwa mara kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii, akibainisha kuwa sio mara ya kwanza kwao kusaidia ujenzi na maendeleo ya kituo hicho cha polisi.

Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuimarisha amani na utulivu katika eneo la Tegeta A na maeneo jirani.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Tegeta A, Nora Gewe, akipokea msaada wa feni kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Bajaji Goba Mpakani, Magawa Augustino, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya madereva wa bajaji na Jeshi la Polisi katika kudumisha usalama na huduma bora kwa jamii.


No comments:

Post a Comment

Pages