Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Chama cha Madereva wa Malori na Mabasi Tanzania kimekanusha taarifa zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii kwa kudai kuwa madereva wa Malori na Mabasi wanajiandaa kufanya mgomo Julai Mosi Mwaka huu,nakwamba hakuna mpango wowote wa kusitisha shughuli za usafirishaji nchini.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa chama hicho Hassan Dede wakati akizungumza na wanahabari,nakusema kwamba madereva wa masafa marefu wanaendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida na hawana nia ya kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuathiri shughuli za kiuchumi au kurudisha nyuma juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukuza uchumi wa taifa.
Amesema kuwa sekta ya usafirishaji ni mhimili muhimu wa maendeleo ya nchi na kwamba madereva wana wajibu wa kuhakikisha huduma za usafirishaji zinaendelea kutolewa kwa ufanisi ili kuchochea biashara na uwekezaji.
“Tunatambua mchango mkubwa wa Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara,uwekezaji na usafirishaji. Hivyo hatuko tayari kushiriki katika jambo lolote litakalovuruga juhudi hizo au kuathiri ustawi wa uchumi wa nchi yetu,” amesema Dede.
Aidha,amesema chama hicho kinaendelea kuhamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa zilizopo nchini Tanzania kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika katika miundombinu na mazingira ya uwekezaji.
Kuhusu taarifa za mgomo zinazoenezwa na baadhi ya makundi na vyama mbalimbali,ikiwemo kile kinachojiita Chama cha Ukombozi, Mwenyekiti huyo amesema kwamba chama chake hakijahusishwa kwa namna yoyote na mipango hiyo na hakijatoa wito wa mgomo kwa wanachama wake.
Pia amewataka madereva wote nchini kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani,umoja na utulivu wa taifa,ikiwemo kushiriki maandamano au shughuli nyingine zinazopangwa kupitia mitandao ya kijamii bila kufuata taratibu za kisheria.
Amesisitiza kuwa amani na utulivu ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, hivyo kila mwananchi anapaswa kushiriki katika kuilinda kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amewataka madereva wa Malori na Mabasi kutojihusisha katika madamano yanayopangwa kufanyika tarehe 7,7,2026 mwaka huu,kwani maandamano hayo ya lengo la kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani Nchini.





No comments:
Post a Comment