Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Benki ya CRDB imedhamini Grand Bunge Bonanza 2026 kwa Shilingi milioni 450, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuendelea kuunga mkono michezo, afya na ustawi wa jamii nchini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya sehemu ya vifaa vya michezo yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Ester Mwambapa, alisema udhamini huo unaakisi dhamira ya benki hiyo katika kuwekeza kwenye afya, ustawi wa jamii pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali.
Alisema Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia mipango yenye manufaa kwa jamii, ikiwemo michezo ambayo imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha afya na kujenga mshikamano miongoni mwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Grand Bunge Bonanza 2026, Festo Sanga, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa mdhamini mkuu wa bonanza hilo, akibainisha kuwa mchango huo umeongeza kasi ya maandalizi ya tukio hilo muhimu.
Sanga alisema bonanza hilo lina lengo la kuhamasisha afya bora, kuimarisha mshikamano na kujenga mahusiano mema kati ya washiriki kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Grand Bunge Bonanza 2026 linatarajiwa kufanyika Juni 20, 2026 katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, likiwakutanisha wabunge, watumishi wa Bunge, wizara, taasisi za serikali na wadau mbalimbali katika michezo pamoja na shughuli za afya.
Tukio hilo linatarajiwa kuwa fursa ya kukuza ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuhimiza umuhimu wa afya kupitia ushiriki wa michezo na mazoezi ya mwili.




No comments:
Post a Comment