HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

June 24, 2026

HAND IN HAND YAZINDUA MRADI WA SHILINGI BILIONI 2. 8 KUINUA UCHUMI WA WANANCHI IRINGA

NA DENIS MLOWE, IRINGA


SHIRIKA la Hand in Hand Eastern Africa Tanzania (HIHEA) limezindua rasmi utekelezaji wa mradi wa Inua 2  mkoani Iringa, likitarajia kuwafikia wananchi 8,000 kupitia mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara, na uboreshaji wa shughuli za uzalishaji katika sekta za kilimo na ufugaji.


Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Ukumbi wa Gentle Hills mjini Iringa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Elia Luvanda alisema ujio wa shirika hilo unaongeza nguvu katika juhudi za serikali za kuharakisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo.

Luvanda alisema serikali ina matarajio makubwa kwamba Hand in Hand itasaidia kuimarisha vikundi vya wananchi kwa kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa mipango ya biashara, uongozi wa vikundi, utunzaji wa kumbukumbu na usimamizi wa shughuli za uzalishaji.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wanufaika kuwa tayari kupata huduma za kifedha kutoka taasisi mbalimbali pamoja na mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

“Tunawakaribisha na tuko tayari kutoa ushirikiano wote unaohitajika na serikali imewaelekeza viongozi wa ngazi zote kuhakikisha shirika hili linapata mazingira mazuri ya kufanya kazi na kuwafikia wananchi waliokusudiwa,” alisema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hand in Hand Eastern Africa Tanzania, Jane Richard Sabuni, alisema shirika hilo limetenga bajeti ya bilioni 2.8 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya fedha hizo zitaelekezwa moja kwa moja kwa shughuli za kuwawezesha walengwa.

Sabuni alisema mradi huo unalenga kuongeza kipato cha kaya kwa kiwango kikubwa kupitia biashara endelevu, kilimo chenye tija, ufugaji na shughuli nyingine za uzalishaji zitakazochaguliwa na wanufaika kulingana na mazingira yao.

Alifafanua kuwa kuwajengea uwezo wanufaika hakutakuwa kwa njia ya mafunzo ya darasani pekee, bali kutahusisha mashamba darasa, wakulima na wafugaji wa mfano, pamoja na ushiriki wa wataalamu wa sekta mbalimbali watakaowasaidia wananchi kuongeza tija katika shughuli zao.

Sabuni alisema Hand in Hand haitatoa mikopo ya fedha moja kwa moja kwa wanufaika, bali itakuwa kiungo kati ya wafanyabiashara wadogo na taasisi zinazotoa huduma za kifedha baada ya kuhakikisha wamepata mafunzo, wameandaa mipango ya biashara na kutimiza masharti yanayohitajika.

“Tunalenga kuwafikia wananchi 8,000 na kuona maisha yao yanabadilika kupitia ongezeko la kipato, biashara endelevu na fursa za ajira. Mafanikio ya mradi huu yatatokana pia na ushiriki wa wananchi wenyewe katika kutumia maarifa watakayopata,” alisema.


Meneja wa Hand in Hand Tawi la Iringa, Amos Kasanga, alisema utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo utaanza katika Manispaa ya Iringa na Wilaya ya Iringa, ukihusisha kata 12 na walengwa wapatao 4,000.

Alisema baada ya kukamilika kwa awamu hiyo, shirika litapanua shughuli zake na kufikia maeneo mengine ikiwemo Wilaya ya Kilolo pamoja na kuongeza idadi ya kata zitakazoshiriki katika mpango huo.

Kasanga alieleza kuwa wanufaika watapitia mafunzo ya miezi 11 yatakayojumuisha elimu ya biashara, utambuzi wa fursa za kiuchumi, usimamizi wa shughuli za uzalishaji na namna ya kuunganisha bidhaa zao na masoko.
Aliongeza kuwa uteuzi wa wanufaika utafanyika kupitia vikundi vilivyopo katika vijiji na kata mbalimbali, ambapo shirika litashirikiana na viongozi wa serikali za mitaa kubaini mahitaji yaliyopo na kutoa msaada unaolenga kuimarisha shughuli za kiuchumi za wananchi.

Kupitia mradi huo, Hand in Hand inatarajia kuchochea ukuaji wa uchumi wa kaya, kuongeza ajira na kupunguza umaskini kwa kuimarisha uwezo wa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na biashara zenye tija.




No comments:

Post a Comment

Pages