Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema kuwa ana kila sababu ya kuwashukuru wanariadha na Watanzania wanaojitokeza kushiriki mbio za CRDB Bank Marathon, kwani ada wanazolipia kujisajili imekuwa chanzo cha kuokoa maisha ya watoto na akina mama wenye mahitaji ya matibabu ya kibingwa.
Dkt. Nsekela alisema huo ndiyo mfano halisi wa ujumuishi wa kijamii ambao Benki ya CRDB imeendelea kuuenzi kwa kuhakikisha kila mwananchi anakuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazowakabili wengine.
Alisema katika misimu sita ya mbio hizo, mamia ya watoto wenye changamoto za moyo pamoja na akina mama wenye ujauzito hatarishi wamefanikiwa kupata matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na CCBRT kupitia fedha zinazokusanywa na mbio hizo, huku familia nyingi zikiwa zisingeweza kumudu gharama za matibabu hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, alisema taasisi hiyo kwa sasa ndiyo kinara wa huduma za matibabu na upasuaji wa moyo Afrika Mashariki, mafanikio ambayo yamechangiwa pia na ushirikiano wake na Benki ya CRDB.
Dkt. Kisenge aliongeza kuwa kuelekea CRDB Bank Marathon ya mwaka huu, wananchi wote watakaoshiriki watapata huduma za uchunguzi wa afya ya moyo bila malipo katika vituo vya JKCI vilivyopo Upanga, Dar Group, Oysterbay, Kawe na Arusha.
Awali, Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Joycelean Makule, alisema tangu kuanzishwa kwa CRDB Bank Marathon, tukio hilo limekuwa zaidi ya mashindano ya riadha, bali ni jukwaa la kugusa maisha ya Watanzania kwa kuunganisha watu na kurejesha kwa jamii.
Alisema kupitia mbio hizo, benki imechangia kwa kiasi kikubwa sekta ya afya kwa kusaidia taasisi zinazotoa huduma za kibingwa kwa watoto, akina mama na wananchi wasioweza kumudu gharama za matibabu, hususan JKCI na CCBRT.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation na Mwenyekiti wa CRDB Bank Marathon, Tully Mwambapa, alisema mbio za mwaka huu zitafanyika Agosti 16, 2026 katika Viwanja vya TTCL Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba.
Alisema eneo hilo litatoa nafasi ya kupokea washiriki wengi zaidi na kuongeza ubunifu katika shughuli mbalimbali zitakazoambatana na mbio hizo.
"Tunakusudia kuendelea kuziinua CRDB Bank Marathon na kuzifikisha katika viwango vya marathon kubwa duniani kama Dubai, Boston, London, Tokyo na New York," alisema Tully.
Aliongeza kuwa mbio hizo zimeendelea kujijengea umaarufu kutokana na kuunganisha michezo, utalii, burudani na utamaduni.
Katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi, Benki ya CRDB pia imezindua tamasha la kimataifa la burudani lijulikanalo kama Imbeju – Sauti Moja, litakalofanyika Agosti 14, 2026 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya CRDB Bank Marathon.




No comments:
Post a Comment