NA EDITHA WILLIAM, KAGERA
Wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Kagera wameaswa kuongeza uwajibikaji na usimamizi wa karibu wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha za Serikali zinaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Wito huo umetolewa katika warsha iliyoandaliwa na TAKUKURU kuhusu wajibu wa wadau katika usimamizi na utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Ramadhani Kido, amesema Serikali inatarajia kuona kila mdau anasimamia kwa karibu miradi inayotekelezwa katika eneo lake na kuchukua hatua za haraka pindi changamoto zinapojitokeza.
Kwa upande wake, kiongozi wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera amesema usimamizi shirikishi kupitia mfumo wa PETS umeendelea kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma kwa kuhakikisha miradi inakidhi viwango vya ubora na kuwanufaisha wananchi.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2023 hadi 2026, TAKUKURU imefuatilia miradi 258 mkoani Kagera, kubaini miradi 26 yenye viashiria vya rushwa, kutoa mapendekezo ya maboresho katika miradi 207 pamoja na kutekeleza programu 242 za uhamasishaji na elimu kwa umma kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.
Warsha hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za Serikali na TAKUKURU za kuimarisha uwajibikaji, kuongeza uwazi na kuhakikisha kila shilingi ya umma inaleta thamani kwa maendeleo ya wananchi.






No comments:
Post a Comment