NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Abdulmajid Nsekela, amewataka wafanyakazi wa benki hiyo kutumia kikamilifu CRDB Fitness Center kwa lengo la kuimarisha afya, nguvu na ufanisi kazini.
Dk. Nsekela ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa CRDB Fitness Center, akisisitiza kuwa kituo hicho hakipaswi kuishia kuwa programu ya Idara ya Rasilimali Watu au tukio la uzinduzi pekee, bali kiwe sehemu ya utamaduni wa wafanyakazi wote wa CRDB.
“Ningependa kuona kwamba tulichokuja kufanya leo kinajenga afya ya wafanyakazi,” amesema Dk. Nsekela.
Amesema matumizi ya kituo hicho yanaweza kusaidia wafanyakazi kupunguza msongo na foleni za matumizi ya muda, huku wakitenga muda wa kujenga afya na uimara wa miili yao.
Amesisitiza kuwa CRDB yenye nguvu inaanza na wafanyakazi wenye nguvu na afya bora, ambao hujenga timu bora, timu hiyo hujenga benki bora na hatimaye benki bora huchangia katika kuboresha maisha ya wananchi na kujenga uchumi.
Dk. Nsekela pia ameitaja nafasi ya CRDB katika kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, akisema sekta ya fedha ni muhimu katika kuwezesha sekta binafsi kupitia mitaji, mifumo ya malipo, teknolojia na ubunifu.
Amesema CRDB inalenga kuwa kinara katika kuunga mkono maono hayo, akieleza kuwa mafanikio hayo yanawezekana kupitia weledi, uwezo, ubunifu na maarifa ya wafanyakazi wake.
“Ninaliona hilo linawezekana kupitia weledi, uwezo, ubunifu na akili za wafanyakazi wetu,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Godfrey Rutasingwa, amesema uzinduzi wa kituo hicho ni mwanzo wa safari ya kuboresha afya za wafanyakazi na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za benki.
Amesema programu hizo zinalenga kuongeza nguvu na uchangamfu wa wafanyakazi, jambo litakalosaidia kuongeza tija katika utendaji kazi.
“Tunaanza safari ya kuboresha afya zetu kutoka hapa tulipo kwenda kwenye nafasi nyingine kubwa zaidi. Tunataka kutoka kwenye productivity tuliyonayo kwenda kwenye productivity kubwa zaidi kwa sababu tutakuwa na afya, nguvu na uchangamfu,” amesema Rutasingwa.
Rutasingwa pia amewataka wafanyakazi kujiunga na klabu mbalimbali za michezo na mazoezi zilizopo ndani ya benki hiyo, akisema tayari zaidi ya wafanyakazi 400 wanashiriki katika klabu hizo.
Amesema uongozi wa benki umeweka utaratibu wa kuhamasisha wafanyakazi kushiriki katika programu hizo, huku akiwataka wafanyakazi wengine kujiunga ili kunufaika na fursa hiyo ya kuimarisha afya na kuongeza tija kazini.









No comments:
Post a Comment